mtoto.news

Kenya: Chanjo ya Covid-19 kwa Watoto Yapigwa Marufuku

June 23, 2022

Mahakama kuu jijini Nairobi imepiga marufuku kwa serikali kutoa chanjo dhidi ya Covid-19 kwa watoto walio chini ya miaka 18 pasipo na ruhusa ya wazazi wao.

Jaji Anthony Mrima alitoa maagizo hayo katika kesi iliyofunguliwa na wazazi 11 ambao walidai kuwa hawakushauriwa wala kuombwa ridhaa kabla ya watoto wao kupewa chanjo.

Kufuatia agizo hilo, Wizara ya Afya italazimika kusitisha mipango yake ya kusambaza chanjo nyingi kwa watoto shuleni na sehemu za ibada.

Katika kesi hiyo iliyowasilishwa na kundi linaloongozwa na Bw Winfred Otieno, mahakama ilisikia kwamba kuna hatari ya watoto kulazimishwa kuchanjwa Covid-19 bila idhini kutoka kwa wazazi wao.

Wakili wa walalamishi Bw Harrison Kinyanjui alisema kwamba, shule, makanisa na sehemu za kazi hazijatangazwa kwenye gazeti la serikali, kwa hivyo haziwezi kutumika kama vituo vya chanjo.

“Wizara inalenga kuwashurutisha watoto hawa kukwepa, kupuuza na kukiuka idhini ya lazima inayohitajika kisheria kwa wazazi na walezi wanaowajibika kisheria kwa vijana hawa kabla ya kutoa chanjo zozote za Covid-19,” alisema Bw Kinyanjui.

Mapema mwezi huu, wizara ya Afya ilitangaza kuwa, serikali itaongeza kasi ya chanjo ya Covid-19 ambayo inafaa kuchukuwa wiki sita. 

Walengwa walikuwa watoto wanaokwenda shule wenye umri wa zaidi ya miaka mitano. 

Nyaraka za mahakama zilisema kuwa, lengo lilikuwa kufikia vijana 800,000 wanaokaribia kujiunga na vyuo vikuu.

Walalamishi hao, ambao pia ni pamoja na Tume ya Haki za Kibinadamu ya Kenya (KHRC) na Kituo Cha Sheria, wanadai kuwa kampeni hiyo inahusisha vihisi nano ambavyo vinadaiwa kuwabadilisha wale wanaodungwa kuwa kama vifaa vya Bluetooth.

Kulingana na wao, chanjo hizo zina athari ya kubadilisha DNA ya binadamu. Waombaji wengine ni Enock Aura, Eliud Karanja, Mbarak Hamid, Dkt Reginald Oduor, Michael Mumo, Michael Otieno, Christine Mugure, Susan Mbugua, Edah Beuttah na Mary Riungu.

Pia waliikosoa serikali kwa kushindwa kutekeleza uhamasishaji kabla ya kutekeleza zoezi hilo.

“Vitendo kama hivyo kwa upande wa Wizara ya Afya vitajumuisha usimamizi wa kulazimishwa wa chanjo ya Covid-19 kwa watoto wa shule wenye afya kabisa, ambayo inahatarisha afya na usalama wao katika hatari ya kifo, majeraha, ulemavu hasa ule wa kudumu,” Bw Kinyanjui alisema.

aliongeza kusema kuwa, kuchukua chanjo inapaswa kuachiwa uamuzi wa watoto na wazazi wao .

Alidai kuwa, hadi sasa, hakuna uthibitisho wa kitabibu kwamba jabs za Covid-19 zina uwezo uliothibitishwa kisayansi wa kuzuia ugonjwa wowote.

Hey, like this? Why not share it with a buddy?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *