mtoto.news

Watoto Milioni 8 Wako Katika Hatari ya Kufariki Kutokana na Utapiamlo

June 28, 2022

Kulingana na ripoti ya UNICEF Takriban watoto milioni 8 walio chini ya umri wa miaka 5 wako katika hatari ya kufa kutokana na utapiamlo mkali.

Kulingana na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, bei ya vyakula imepanda kwa kasi mwaka huu kutokana na vita vya Ukraine, huku ukame unaohusishwa na mabadiliko ya hali ya hewa katika baadhi ya nchi na janga la COVID-19 zikishika kasi.

Wengi wa watoto hawa wako katika nchi 15 zinazokumbwa na uhaba mkubwa wa chakula na msaada wa matibabu. 

Nchi hizi zilizokumbwa na mzozo ni pamoja na Afghanistan, Ethiopia, Haiti na Yemen.

Ukosefu wa lishe husababisha kupungua kwa kinga ya mwili, ambayo huongeza hatari ya kifo hasa kwa watoto walio chini ya miaka 5.

Ripoti ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto ilisema kwamba, utapiamlo umeathiri watoto zaidi ya 260,000 tangu mwanzoni mwa mwaka wa 2022. Idadi inayoongezeka kila siku.

Bei ya vyakula imekuwa ikipanda kwa kasi kutokana na vita vya Ukraine na ukame unaoendelea kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa katika baadhi ya maeneo ya dunia. 

Athari za kiuchumi zinazoendelea za COVID-19 pia zimechangia kuongezeka kwa visa vya utapiamlo miongoni mwa watoto.

Advertisements

REPORT THIS AD

UNICEF imesema kwamba, kifurushi cha msaada cha dola bilioni 1.2 kinahitajika haraka ili kuweza kushughulikia mzozo unaokuja.

Aidha nchini Kenya bei ya vyakula vya kimsingi vimepanda juu mno, huku wimbi la sita la COVID 19 likichacha.

Upande wa Somalia Mogadishu, Hospitali zinalemewa na ongezeko la watoto wenye utapiamlo, hii ikiashiria wazi kwamba, Somalia inaelekea kwenye baa la njaa ambalo linaweza kuua mamia ya maelfu.

Huku vitanda vikiwa vimejaa na wodi zikiwa zimeharibika, madaktari wanalazimika kuhudumia watoto katika mahema, vyumba vya mikutano na hata kwenye magodoro yaliyowekwa nje, huku ukame katika Afrika Mashariki na vita vinavyoendelea nchini Ukraine vikipandisha bei ya vyakula, na kufanya chakula cha msingi kuwa ngumu kwa mtu kumudu.

Cha kusikitisha ni kwamba, idadi ya watoto wanaofariki katika kituo hicho pia inaongezeka huku wengi zaidi wakifika wakiwa wamekabiliwa na utapiamlo na magonjwa mengine. 

Kulingana na Save the Children, Watoto wanane walikufa huko ndani ya mwezi Mei peke yake.

Njaa nchini Somalia inaongezeka kwa kasi zaidi kuliko ilivyohofiwa hapo awali.

Watu wanalemewa na mchanganyiko mbaya wa mambo ambayo yanaenda mbali zaidi ya yale tuliyoona mwaka wa 2011, ambapo watu 250,000 walikufa. Familia nchini Somalia ziko kwenye hatari ya mawimbi makali ya dunia.

 MOHAMUD MOHAMED HASSAN MKURUGENZI WA SHIRIKA LA SAVE THE CHILDREN NCHINI SOMALIA

Tangu mwaka huu uanze, zaidi ya watu 500,000 wamehama makazi yao, wakiwa wamedhamiria kutafuta chakula, maji na huduma za afya zitakazowasaidia wao na watoto wao kujikimu kimaisha.

Binti ya Astur* mwenye umri wa miaka minne alikabiliwa na utapiamlo na surua kabla ya yeye na familia yake kufunga safari ngumu hadi Baidoa, ambapo watoto tisa kati ya kumi wanakabiliwa na utapiamlo mwaka huu. 

“Kwa miaka minne, hatujaona mvua. Tulipoteza wanyama wetu na hakuna kitu kinachokua katika shamba letu. Hatukuweza kuvumilia zaidi na ndiyo maana tuliondoka kwenda Baidoa kutafuta msaada. Tulikuwa tunaona vipindi vya ukame hapo awali, lakini sio ukame mbaya kama huo.”

ASTUR

Astur alitembea kwa kilomita 90 kwa siku mbili mchana na usiku, huku watoto wake wawili wenye utapiamlo wakibebwa kwenye toroli ya punda. 

Juhudi za kufika Baidoa huenda ziliokoa maisha* ya bintiye Yasmiin aliye na miaka miwili. Siku moja baada ya wao kufika, timu ya lishe ya Save the Children iliwakimbiza kutoka kambi iliyokuwa ishajaa hadi hospitali iliyofurika ambapo kila kitanda kilikuwa kimelaliwa kwa wiki kadhaa. 

Madaktari walilazimika kuwatunza Yasmiin na Astur chini ya mti hadi kitanda kitakapoweza kupatikana, ambayo ilikuwa baada ya masaa machache.

Wafanyikazi wa afya wa Save the Children walisema kwamba, pasipo na matibabu, Yasmiin hangekuwa na uwezekano wa kuishi wiki hiyo.

Hakuna muda wa kupoteza, lazima watoto washughulikiwe kwa haraka, kwani wanahitaji Lishe Bora na Afya Njema.

Hey, like this? Why not share it with a buddy?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *