“Wanasiasa hutuhusisha kwenye siasa pale tu wanapotaka kuzusha vurugu, hapo ndipo wanakuja na pesa huku wakitutaka tuanzishe ugomvi mahali fulani.”
Wycliffe mtoto kutoka maeneo ya Dandora, Jijini Nairobi analalamika jinsi wanasiasa hawawashughulishi watoto kwenye mchakato wa uchaguzi, au kuwahusisha kwa mambo yenye manufaa, kama vile kutaka kujua shida zao za kimsingi, Ila wanasiasa hawa huwapatia watoto pesa kidogo kidogo huku wakiwashauri waende kuanzisha zogo au mizozo mahali fulani.
Mizozo ambayo huwaweka watoto hawa katika hatari ya majeruhi na hata saa zingine vifo.
Mara nyingi, wanasiasa hawa huwatembelea watoto wanaoishi katika mazingira magumu zaidi au waliotoka katika jamii maskini, wakiwaahidi pesa kidogo kwa ajili ya kuchochea vurugu.
Watoto ambao hawajui penye watatoa chakula wala hawajui penye watalala, na hivyo wanaona kuwa hiyo ni nafasi nzuri kwao kupata pesa ya haraka, kwani dau la mnyonge haliendi joshi, na mtu hujikuna ajipatapo.
Katika miaka ya hivi karibuni, zaidi ya watoto milioni 20 wameyakimbia makazi yao na zaidi ya watoto milioni 2 wamejeruhiwa vibaya au wamekufa duniani kote kutokana na kukabiliwa na migogoro ya silaha na aina nyingine za ukiukaji wa haki za binadamu (UNICEF, 2011).
Vurugu kabla ya uchaguzi na baada ya uchaguzi huwaathiri watoto sio tu kimwili, bali pia kisaikolojia.
Kuna haja kuu ya kuwalinda watoto dhidi ya ukatili, hasa katika kipindi hichi cha uchaguzi.
Hakuna maisha yanayopaswa kupotea au kujeruhiwa kwa sababu ya Uchaguzi.
Kila mtu anafaa ajizatiti kuwalinda watoto, ikiwemo wanasiasa, mashirika ya kijamii, serikali, wazazi, na hata mtu yeyote yule.
kwenye video hii utaweza kusikia mjadala unaoashiria zaidi jinsi watoto wanavyohusishwa wakati wa uchaguzi nchini kenya,
Leave a Reply