mtoto.news

Wazazi wa Watoto Viziwi Waomba Mahitaji Maalum Ya Elimu

July 18, 2022

Wazazi walio na watoto viziwi katika Kaunti ya Mombasa wamezindua Shirika la Jamii litakalotetea haki za watoto wao ikiwemo elimu na huduma za afya.

Wanachama wa Pamoja Parents for Deaf CBO wametoa wito kwa serikali ya kitaifa kufikiria kujenga shule ya upili ambayo itashughulikia mahitaji ya elimu ya msingi ya watoto wao.

Walilalamika kwamba, kuna ukosefu wa shule kamili ya sekondari ya umma katika kata hiyo ya wanafunzi wenye ulemavu, hii ikiwalazimu wao kuwapeleka watoto wao mbali licha ya uhitaji wao mkubwa wa malezi ya karibu ya wazazi.

Wanandoa, Daniel Anyazwa na Stella Habela, ambao wana watoto wanne wenye matatizo ya kusikia walisema kuwa, kuwapeleka watoto wao katika shule za mbali ni vigumu mno, kwani hawana uwezo wowote wa kifedha wa kuweza kuwapeleka mbali.

“Shule za karibu zinazohudumia watoto wetu ziko katika kaunti za Kilifi na Kwale ambazo pia zina changamoto zao ikiwemo malazi. Ilitubidi kuchimba sana mifuko yetu ili kuwapeleka shule za mbali” alisema Habela.

Wanandoa hao kutoka eneo la Kwabulo eneo bunge la Nyali walio na wana watatu wa umri wa miaka 25, 24 na 8 na binti wa miaka 13 waliongeza kusema kwamba, matatizo ya kifedha yalitatiza juhudi zao za kusomesha watoto wao.

Mildred Sigunda na Florence Kasichana, Mama wawili walio na watoto walemavu wanakumbwa na matatizo yayo hayo.

Mildred, mama wa watoto watatu akiwemo mmoja aliye na matatizo ya kimwili na kiziwi aliomba serikali ya kitaifa na serikali ya kaunti kutoa huduma zitakazosaidia elimu ya watoto wao.

“Watoto wetu wanastahili elimu na huduma za matibabu kama watoto wengine wowote wa Kenya. Tunahitaji shule maalum za umma za msingi na sekondari zilizo na vifaa vinavyokidhi mahitaji ya elimu ya watoto wetu,” aliongeza Mildred.

Kasichana, mkazi wa Kisauni na mama mzazi wa mtoto kiziwi amelilia suala la ukosefu wa wakalimani wa lugha ya ishara katika hospitali za umma, kwani hii yaleta changamoto kubwa kwa jamii ya viziwi mjini Mombasa.

Alitoa wito kwa serikali ya kaunti kuzingatia kuajiri wakalimani waliofunzwa ambao wanaweza kufanya kazi na kuhudhuria, kutambua magonjwa ya wagonjwa viziwi wanaotembelea vituo vya umma.

“Mtoto wangu mkubwa amekataliwa mara kadhaa kwa sababu ya kukatika kwa mawasiliano na nisipofuatana naye hatahudumiwa ipasavyo,” aliongeza Kasichana.

Abdulswamad aliahidi kuinua jamii ya viziwi na wanajamii wengine wenye ulemavu wa aina nyingine.

Aidha aliihakikishia jamii kuwa, atashirikiana na wadau wengine kuzipatia ufumbuzi baadhi ya changamoto zinazowakabili kwa sasa katika upatikanaji wa afya na elimu kwa watoto wao.

“Nitaendelea kuwaunga mkono hasa kupitia ufundi cherehani, uchomeleaji, uashi ambao ungewawezesha kuanza shughuli za kujiongezea kipato,” aliongeza.

Takwimu zinaonyesha kuwa kuna watoto 200,000 viziwi wenye takriban asilimia 10 tu ya masomo.

Nchi ya kenya ikiwa na shule 120 zikiwemo shule za sekondari 23 za wanafunzi viziwi.

Hey, like this? Why not share it with a buddy?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *