mtoto.news

Sanduku la Malalamishi la Kushughulikia shida za Watoto

July 22, 2022

Shirika Lisilo la Kiserikali (NGO) linalojulikana kama Kamati ya Kimataifa ya Maendeleo ya Watu (CISP), limeunda visanduku vya mazungumzo na vilabu vya kutetea haki za watoto katika shule mbalimbali mjini Kakamega, ambapo watoto wanaweza kueleza shida ambazo wanataka zishughulikiwe.

Meneja wa programu wa CISP, Esther Waduu, amesema kwamba, vilabu vya kutetea haki za watoto vina umuhimu kwani vinabadilisha tabia za watoto na uelewa wao kuhusu haki zao.

“Vilabu hivi, vinawasaidia watoto hawa kujua mahali pa kutafuta msaada na kuhakikisha haki zao zinalindwa na ziko mstari wa mbele katika kuripoti kesi za ukiukwaji wa haki zao,” alibainisha.

Watoto pia huweza kubadilishana mawazo kupitia vikao vya rika moja, hii ikiwawezesha kutoa mafunzo kwa watoto walio katika shule zingine, kuhusu stadi za maisha.

“Ni muhimu sana katika kujenga ujasiri wa watoto kuzungumza wanaponyanyaswa,” alibainisha.

Sanduku la mazungumzo ni mfumo mno, kwani watoto hupewa sauti ya kuripoti masuala yanayowahusu kwa kudondosha karatasi yenye malalamiko au masuala yao ndani ya kisanduku.

Kamati inayojumuisha mwakilishi wa wazazi, mwalimu, afisa wa ulinzi wa mtoto na mshauri nasaha hufungua sanduku kila mwezi, na hupitia malalamishi yaliyopo na kisha kuzielekeza idara mbalimbali ili hatua zichukuliwe.

“Tunawahimiza watoto kuwaendea walimu wao hasa katika masuala ambayo yanahitaji uingiliaji kati wa haraka kwani iwapo malalamishi hayo yatawekwa kwenye sanduku ambalo hufunguliwa mara moja kwa mwezi, basi afueni yaweza kuchelewa,” alisema.

Shirika hili la CISP linashirikiana na Chuo Kikuu cha Kenyatta, Matungu Rural Poverty Alleviation(MARP), Kenya National Outreach, Counseal and Training Program(K-NOTE), Serikali ya Kaunti ya Kakamega, Wizara ya Afya na Wizara ya Elimu.

Kwa kuongezea, CISP imeshirikiana na kampuni ya kibinafsi nchini Italia katika kuunda Mfumo wa Usimamizi wa Watoa Huduma (SPMS), ili kuhakikisha ufikiaji rahisi na utoaji huduma kwa watoto wote.

Hey, like this? Why not share it with a buddy?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *