mtoto.news

Kufungwa Ghafla kwa Shule Kumewatatiza Wazazi

August 2, 2022

 

Wazazi ambao wamelazimika kutafuta nauli ya safari za watoto wao kurudi nyumbani, wamesikitishwa na agizo la kufungwa kwa shule hii leo, huku wakieleza kuwa hatua hiyo ni ya kutozingatia.

Baadhi yao wamejitokeza kwenye mitandao ya kijamii na kumkashifu Waziri kwa agizo hilo, Kwani ahadi ya awali ilikuwa ni kwamba, shule zilitarajiwa kufungwa ijumaa tarehe 6 na hivyo tangazo hilo la kufungwa tarehe tatu lilikuwa mshtuko kwa wazazi wengi.

“Prof. George Magoha alijua kwa miaka mingi kwamba uchaguzi ungefanyika tarehe 9/8 na hivyo shule zingetumika kama vituo vya kupigia kura! Mkanganyiko unaoletwa na maagizo yake kwa kweli hauhitajiki! Ndiyo maana tunahitaji maafisa wa serikali ambao wanawasiliana na wananchi,” Mbunge wa Molo Kuria Kimani alisema.

“Magoha amesababisha hofu isiyo ya lazima katika sekta ya usafiri kwa watoto wanaorudi nyumbani leo. Nilikuwa nimeweka tikiti ya kaka yangu ya treni wiki zilizopita, Ila baada ya tangazo la Magoha hapo jana, treni imeshajaa na sasa inabidi tutafute njia nyingine za yeye kufika nyumbani.,” alisema Pmusesya mtumiaji wa twitter.

Waziri Magoha hapo awali alidokeza kwamba taasisi hizo zitafungwa kuanzia Jumamosi lakini akaeleza kuwa uamuzi wa kuzifunga mapema ulitokana na mashauriano ya zaidi.

Alisema kwamba, kufungwa huko kutahakikisha kuwa maandalizi na uendeshaji wa uchaguzi ujao unafanyika bila vikwazo, akibainisha kuwa shule nyingi zitakuwa vituo vya kupigia kura.

Waziri pia alibainisha kuwa tarehe ya kurudi shule ni Agosti, 10 ila tarehe hizo zinaweza kurekebishwa iwapo uchaguzi wa marudio utafanyika.

Magoha alikiri kwamba, kalenda ya mitihani ya kitaifa inaweza kuathirika.

Mwaka wa masomo wa 2022 una mitihani minne ya kitaifa huku Cheti cha Kenya cha Elimu ya Msingi na Cheti cha Elimu ya Sekondari cha Kenya kikitarajiwa kufanyika kati ya Novemba 28 na Desemba 23.

Baraza la Kitaifa la Mitihani la Kenya lilitangaza kuwa litafungua tovuti kuanzia Agosti 15 hadi Agosti 30 ambapo wanafunzi wa darasa la 6 watachagua Shule za Upili wanazopendelea kabla ya mtihani wa kitaifa.

 

Hey, like this? Why not share it with a buddy?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *