mtoto.news

Ahukumiwa Kifungo cha Miaka 100 kwa Kunajisi Watoto

August 5, 2022

Mkurugenzi wa Children’s home ambaye alishtakiwa kwa kosa la  kuwanajisi wavulana chini ya uangalizi wake amehukumiwa kifungo cha miaka mia gerezani.

Stephen Nzuki Mutisya amehukumiwa kifungo cha muda mrefu na Hakimu Mkuu Mwandamizi wa Milimani Zainab Abdul ambaye amesema kwamba, vitendo vyake ni vya “kinyama”.

Mutisya amepatikana kuwa, amewanajisi wavulana hao kutoka Scream Africa Child Home na Vijiko School katika mtaa wa Utawala jijini Nairobi kati ya mwaka wa 2010 na 2016.

Waathiriwa hao walikuwa chini ya umri wa miaka 10.

Mahakama ilisikia kwamba Mutisya alikuwa akiwapeleka wavulana hao kwenye makazi yake, kisha akiwapa chakula na vinywaji na baadae kuwahadithia hadithi  za Biblia kabla ya kuwanajisi.

“Wavulana na wasichana wa umri mdogo wanahitaji kulindwa na mahakama dhidi ya wanadamu wasio na huruma,” alisema Bi Abdul hapo jana.

Hakimu alisema kwamba, mahakama imepewa mamlaka na sheria ya kuwalinda wanyonge kwa kutoa hukumu kali dhidi ya watu hao ili iwe funzo kwa wale wanaodhamiria kukiuka haki za watoto.

Kutokana na kuwapotosha wavulana hao kwa kunukuu Biblia na kuwadhulumu kingono, hakimu huyo alisema kwamba, mshukiwa alienda kinyume na mwito wake wa kuwa mfano wa wavulana kutoka katika maeneo duni.

Akitoa hukumu kwa Mutisya, Bi Abdul alizingatia ushahidi uliorekodiwa wa waathiriwa, ambao walikuwa wameitaka mahakama kutoa hukumu ya kuzuia.

“Mahakama imezingatia ripoti ya athari ya waathiriwa ambayo iliwasilishwa mbele ya mahakama hii. Waathiriwa wameishukuru mahakama, ambayo imemtia hatiani mshtakiwa,”

Alipompata na hatia mshtakiwa mwishoni mwa mwezi uliopita, Bi Abdul amesema kwamba, Mutisya alichukua fursa ya watoto hao huku akiwanukuu mistari ya Biblia kwa nia ya kuwashawishi kwamba matendo yake haramu yanaruhusiwa katika Biblia.

Bi Abdul Aliongeza kuwa, mshtakiwa alitambuliwa vyema na waathiriwa wakati wa kesi.

 

Hey, like this? Why not share it with a buddy?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *