mtoto.news

Ukosefu wa Sodo Wachochea Mimba za Utotoni

August 11, 2022

Wakati familia Nyingi zilizo maeneo ya miji zinakabiliwa na uhaba wa unga, wale walio katika maeneo ya vijijini wanalazimika kuchagua kati ya chakula na mahitaji mengine ya kimsingi.

Na kwa sababu mtu hawezi kuishi bila chakula, basi familia hizi hazina budi ila kutupilia mbali masuala mengine kama vile mahitaji ya kimsingi, hii ikiwalazimu watoto wa kike kujitafutia sodo.

Wengi wao hugeuka kutumia pamba, karatasi shashi, gubigubi zilizoraruka na matambara, mwishowe wanaamua kujiingiza kwenye ngono ili waweze kumudu sodo.

“Mfadhaiko tunaopitia kupata pedi hizi ni mwingi,” mwanafunzi katika Shule ya Msingi ya Vihiga alisema.

“Tangu kuzuka kwa Covid, tumekuwa tukihangaika kupata Sodo wakati wa hedhi, kwani wazazi wengi hawawezi kuzimudu.”

Takwimu kutoka kwa Wizara ya Afya mwezi uliopita ziliorodhesha kwamba, Kenya imenyakua nafasi ya tatu katika visa vya mimba za utotoni.

Takwimu hizo, zilizotolewa na Waziri wa Afya, Susan Mochache, ziliashiria kuwa,  msichana mmoja kati ya watano nchini ni mjamzito au tayari amepata mtoto wake wa kwanza.

Ripoti hiyo ilisema zaidi kwamba, angalau watoto 98 wenye umri wa kati ya miaka 10 na 19 wanaambukizwa VVU kila wiki nchini Kenya.

Hata hivyo changamoto ya mimba za utotoni, inawakumba zaidi wasichana katika maeneo ya vijijini.

Ukosefu wa mahitaji muhimu kama vile sodo umewalazimu wengi
kuziba pengo kwa vita dhidi ya mimba za utotoni katika kaunti za mashambani, shirika lisilo la kiserikali la India, Together for Better Foundation, limekuja kuwaokoa wasichana walio katika mazingira magumu ambao hawawezi kumudu Sodo.

Aruna Varsana kutoka Shirika hilo anasema kwamba,njia moja ya kuzuia mimba za utotoni ni kuhakikisha mtoto wa kike anapata mahitaji ya kimsingi, haswa sodo.

Mwanaharakati huyo, ambaye alikita mahema katika kaunti za Kakamega na Vihiga ili kusambaza sodo za bure alisema kwamba, juhudi zinafaa kuelekezwa maeneo ya mashambani.

Wakfu huo umezindua mradi wa taulo za bure bila malipo unaolenga wasichana 1,800 kutoka familia zilizo hatarini katika shule za umma katoka kaunti za Kakamega na Vihiga.

Shule zinazotarajiwa kufaidika na mradi huo wa Sh milioni 1.5 ni pamoja na shule za msingi za Township, Amalemba, Shitaho, St George, Shivakala na Matende huko Kakamega.

Katika Vihiga, ni pamoja na shule za msingi za Kedohi, Chavugami, Navuhi, Vihiga, Chango na Ikumba.

Sodo hizo zasambazwa miongoni mwa wasichana wenye umri wa miaka 12-15 katika shule za msingi ili kuwaendeleza darasani.

Kaunti hizo mbili zilichaguliwa baada ya kilio kutoka kwa umma kwamba wasichana wengi hawawezi kujikimu darasani wakati wa hedhi.

Varsana alisema kwamba, lengo lao ni kuhakikisha kwamba mtoto wa kike analindwa na kupewa nafasi sawa ya kuwa darasani.

“Tunataka kuona wanawake sasa wakiwa mstari wa mbele. Tunaweza tu kufanikisha hilo ikiwa tutawaweka wasichana wetu shuleni,” alisema
“Hatujampuuza mtoto wa kiume kwani tunaanzisha maktaba na kwa sasa zimetimia 45 nchini, ambapo wavulana wetu wanaweza kwenda kusoma bila malipo.”

walimu walipongeza mpango huo wa kusambaza sodo za bure, wakisema utasaidia idadi ya wanafunzi wa kike kuwa darasani.

Hey, like this? Why not share it with a buddy?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *