Kulingana na Save the Children wazazi kutoka kaskazini-mashariki mwa Uganda wanalazimika kuwatuma watoto wao wachanga wa umri wa shule ya awali, shuleni pamoja na ndugu zao ili waweze kushiriki kwenye mlo wa bure shuleni kwani idadi ya familia zisizoweza kumudu chakula nyumbani inazidi kuongezeka.
Natalina, aliye na miaka 10, anasoma katika shule ya jumuiya inayoungwa mkono na Save the Children huko Karamoja, mara nyingi Natalina huenda shuleni pamoja na dada zake wa miaka minne na wa miaka miwili ambaye hubebwa mgongoni mwa Natalina.
Alisema: ” Kila siku ninakuja shuleni na ndugu zangu wawili. Mmoja ana miaka minne na mwingine ana miaka miwili…
Mimi hugawa chakula changu na ndugu zangu wawili kwa sababu bado hawajafikia umri wa kwenda shuleni, na kwa hiyo mimi pekee ndiye hupokea chakula.”
Shirika hilo lilisema kwamba, zaidi ya asilimia 40 ya watu sasa wako kwenye dimbwi la njaa katika eneo la Karamoja, hili ni mojawapo la eneo maskini zaidi na lililotengwa nchini Uganda ambalo kwa kiasi kikubwa lina jamii ya wafugaji,
Karamoja, ambayo inapakana na Kenya na Sudan Kusini, inakabiliwa na mchanganyiko wa hali mbaya ya hewa, magonjwa na mashambulizi ya magenge yenye silaha ambayo yamesababisha zaidi ya watu nusu milioni kwenye viwango vya njaa.
Mwaka jana jamii za Karamoja zilikumbwa na mafuriko na maporomoko ya ardhi.
Hali katika eneo la vijijini kaskazini mashariki imezorota katika miaka ya hivi karibuni.
Shirika la Save the Children limesema kwamba, zaidi ya watoto 91,600 na wanawake 9,500 wajawazito au wanaonyonyesha huko Karamoja wanakabiliwa na utapiamlo na wanahitaji matibabu ya haraka.
Katika Pembe ya Afrika, misimu minne ya mvua iliyofeli imesababisha ukame mbaya zaidi kuwahi kutokea katika kipindi cha miaka 40, na kuwaacha zaidi ya watu milioni 18.6 wakikabiliwa na janga la njaa na utapiamlo ambao unaenea katika ukanda wa Afrika Mashariki hadi Uganda, Sudan Kusini na Sudan.
Aidha, migogoro ya hali ya hewa inafanya matukio ya hali ya hewa kali kama vile ukame na mafuriko ya mara kwa mara na yenye hasara kubwa.
Leave a Reply