mtoto.news

Marsabit: Ukame Watatiza Masomo ya Watoto

August 31, 2022

Ukame mkali katika kaunti ya Marsabit unatatiza masomo ya watoto, huku wengi wao wakilazimika kuacha shule.

Ukosefu wa chakula ni kati ya mambo makuu ambayo huathiri watoto walio chini ya miaka mitano na kusababisha utapiamlo, kudumaa kwa ukuaji na kupungua uzito.

Kulingana na Mamlaka ya Kitaifa ya Kudhibiti Ukame, robo milioni ya watu wanahitaji msaada wa chakula kutokana na ukosefu wa mvua kwa misimu minne mfululizo

 

Uhaba mkubwa wa maji unaoshuhudiwa katika kaunti nzima pia unasababisha upungufu wa maji mwilini miongoni mwa wanafunzi shuleni.

Mkurugenzi wa Elimu katika kata hiyo Titus Mbatha amesema kwamba, elimu katika kata hiyo imeathiriwa kwa kiasi kikubwa na ukame uliopo, kwani wazazi wengi wanategemea mifugo yao kusomesha na kulisha familia zao.

Hata hivyo Mbatha akizungumza na wanahabari katika afisi yake mjini Marsabit siku ya Jumatatu, alisema kwamba idara ya elimu iliiomba NDMA kusambaza maji shuleni.

Alisema kuwa, shule hizo zitapata maji baada ya wiki moja.

Kulingana na Apisho la The Star Mkurugenzi huyo aliwataka wazazi kutowatoa watoto shuleni, huku akisistiza kuwa wameshirikiana na UNICEF  kuanzisha programu za kuwaelimisha wazazi umuhimu wa kuwapeleka watoto shuleni.

Aidha Mbatha amewataka wazazi kuwasimamia na kuwalinda watoto wao, na kuongeza kuwa ni vyema kwa wazazi kuhakikisha watoto wao wanajiepusha na tabia za kutowajibika na uhalifu.

Aliendelea kusema kwamba, wazazi wanapaswa kuhakikisha watoto wao wanazingatia elimu.

Mbatha alisema elimu ni moja ya nyenzo muhimu ambayo mzazi anaweza kuwapa watoto wake.

“Wekeni msingi mzuri kwa watoto wenu kwa kuhakikisha wanapata elimu bora licha ya changamoto za kiuchumi,” alisema.

Aidha Mkurugenzi huyo aliwataka wazazi na walezi wa wasichana waliobaleghe kuwapa uangalizi, ili kuzuia mimba za utotoni na ndoa za utotoni.

Alisema kwamba, majukwaa ya kidijitali yanahitaji umakini wa ziada kutoka kwa wazazi ili kuhakikisha kuwa hayaathiri ukuaji kamili wa watoto wao.

Hata hivyo, Mbatha alisema kuwa, watoto wanaopata mimba wakiwa shuleni, bado wataendelea na masomo.

Vile vile Mbatha aliwasihi wazazi, wajitahidi katika kuwakatisha tamaa wavulana wao kujihusisha na shughuli za bodaboda.

Kwani wengi wao huacha kwenda shuleni, kwa sababu ya kujihusisha na biashara ya bodaboda.

Alisema kwamba, idadi ya wavulana shuleni inapungua tofauti na ile ya wasichana, ambayo inaendelea kuongezeka.

Mkurugenzi huyo alisema serikali imejipanga vya kutosha kwa ajili ya mabadiliko ya Shule ya Sekondari ya Vijana na vyumba vya madarasa vimekamilika. 

 

Hey, like this? Why not share it with a buddy?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *