mtoto.news

Mlipuko wa Surua Zimbabwe, Waua Watoto 700

September 6, 2022

Ugonjwa wa Surua nchini Zimbabwe unaendelea kuwaangamiza watoto.

Wizara ya afya nchini humo imesema kwamba, idadi ya vifo vya watoto vilivyotokana na Ugonjwa huo vimeongezeka hadi karibia 700.

Wengine wanatoa wito wa kutungwa kwa sheria ya kufanya chanjo kuwa ya lazima katika nchi ambayo madhehebu ya kidini ya kupinga dawa za kisasa yanashikilia sehemu kubwa ya watu milioni 15.

Wizara ya afya ya nchi hiyo ya kusini mwa Afrika ilitangaza mwishoni mwa wiki kuwa watoto 698 wamefariki kutokana na surua tangu mlipuko huo uanze mwezi Aprili.

Takwimu za hivi punde ni zaidi ya mara nne ya vifo vilivyotangazwa takriban wiki mbili zilizopita ambapo wizara hiyo ilisema kuwa, watoto 157 ambao wengi wao walikuwa hawajachanjwa kutokana na imani za kidini za familia zao waliugua ugonjwa huo.

Dk. Johannes Marisa, rais wa Chama cha Madaktari na Madaktari Binafsi wa Meno wa Zimbabwe, aliliambia Shirika la Habari la Associated Press siku ya Jumatatu kuwa serikali inapaswa kuongeza kampeni ya chanjo kubwa inayoendelea na kuanzisha programu za uhamasishaji zinazolenga hasa vikundi vya kidini vya kupinga chanjo hiyo.

UNICEF, Jumatatu ilisema kwamba,ina wasiwasi mkubwa na idadi ya kesi na vifo kati ya watoto kutokana na surua. Shirika hilo lilisema linasaidia serikali kukabiliana na mlipuko huo kupitia programu za chanjo.

Ugonjwa wa surua uliripotiwa kwa mara ya kwanza katika jimbo la mashariki la Manicaland mapema mwezi wa Aprili na tangu wakati huo umeenea katika maeneo yote ya nchi.

Vifo vingi vimekuwa vya watoto ambao hawakuchanjwa, Waziri wa Habari Monica Mutsvangwa alisema mnamo Agosti.

Baraza la Mawaziri la Zimbabwe limetumia sheria inayotumika kukabiliana na majanga ili kukabiliana na mlipuko huo.

Serikali imeanza kampeni kubwa ya chanjo inayolenga watoto wenye umri wa kati ya miezi 6 na miaka 15 na inawashirikisha viongozi wa kimila na wa kidini kuunga mkono azma hiyo.

Surua ni miongoni mwa magonjwa ya kuambukiza duniani na huenea zaidi kupitia hewa, haswa kwa kukohoa, kupiga chafya au kugusana kwa karibu.

Dalili ni pamoja na kikohozi, homa na upele wa ngozi.

Surua kali na vifo vitokanavyo na matatizo haya husababishwa na watoto kutopewa chanjo.

Hey, like this? Why not share it with a buddy?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *