mtoto.news

LAMU: Vikundi Vya Walemavu Vyavuna Mpango Wa Elimu Ya Kifedha

September 8, 2022

Angalau Watu 80 walio kwenye Makundi ya Walemavu, kutoka kaunti ya Lamu wanatazamiwa kufaidika na mpango wa elimu ya kifedha, unaolenga kuinua hali yao ya kijamii na kiuchumi.

Mpango huo uliozinduliwa chini ya mwamvuli wa Muslim Women Advancement of Rights and Protection (MWARP) na The Aga Khan Foundation vikundi vitawekwa kupokea ufadhili kupitia wao kuanzisha biashara zao wenyewe kwa nia ya kuhakikisha wanajisimamia wenyewe.

Akizungumza na vyombo vya habari hivi leo kufuatia uzinduzi wa mpango huo katika Makao Makuu ya Kata ya Mokowe, Mkurugenzi Mtendaji wa MWARP Rahma Gulam alisema kuwa mpango huo utapunguza hali ya watu wenye ulemavu ambao wengi wao wameteseka tangu kuanza kwa janga la Covid-19.

“Watu wengi, haswa wasimamizi wa maslahi ya kimsingi kwenye familia, walipoteza kazi zao, huku wategemezi wao ambao ni walemavu wakiteseka mno kwa kutohudumiwa vyema,” alisema.

Gulam aliendelea kusema kuwa mpango huo wa miezi sita ambao utajumuisha utambuzi, usajili, mafunzo na ufadhili wa vikundi hivyo pia utalenga kuhakikisha kuwa watu wenye ulemavu wanazingatiwa katika Mpango wa Maendeleo wa Kaunti (CIDP).

“Pia tuko kwenye mazungumzo na serikali ya kaunti ili kuhakikisha kuwa watu wenye ulemavu wanazingatiwa katika mgao wa bajeti unaoendelea ili kuhakikisha kuwa mahitaji yao ya kijamii na kiuchumi yanazingatiwa,” afisa huyo wa CBO alisema.

Hisia hizi, ziliungwa mkono na ofisa programu wa MWARP, James Chappa ambaye alisema kuwa mpango huo ni jibu la moja kwa moja kwa watu wenye ulemavu, ambao wameteseka mno tangu janga la Covid-19.

Aidha alisema kuwa ufunguo wa mafanikio ya mpango huo unatokana na ushirikiano wa wadau wote ili kuwaondolea unyanyapaa watu wenye ulemavu.

“Kuna haja kwa serikali ya kaunti na ya kitaifa kuhusika katika kuhakikisha kwamba watu wenye ulemavu wanawezeshwa sawa na wakazi wengine kupata fursa zinazojumuisha elimu, kazi na pia miundombinu,” alisema.

Mkurugenzi wa Baraza la Kitaifa la Watu Wenye Ulemavu Joseph Wanjohi kwa upande wake alisema kuwa juhudi shirikishi tayari zinaendelea katika kuhakikisha kuwa watu wote wenye ulemavu wamesajiliwa tena katika jitihada za kuhakikisha kuwa wanapata fursa za hatua za awali ambazo zinapatikana kwao.

Mkurugenzi wa Kaunti ya Huduma kwa Watoto Kaunti ya Lamu Maxwell Titima alidakia kusema kuwa watoto wenye ulemavu wanapaswa kuzingatiwa wakati misaada ya walemavu inasambazwa.

Aidha alisema kuwa Wazazi walio na watoto wenye ulemavu wanatakiwa kuwasajili watoto wao kwa NCPWD mapema ili kuhakikisha kuwa ndugu zao wanazingatiwa kwa ajili ya mipango ya kuwasaidia walemavu.

“Idadi kubwa ya wazazi wamekuwa wakiwaficha watoto wao walio na ulemavu badala ya kuwawezesha kusajiliwa na NCPWD,” Titima alisema.

Hey, like this? Why not share it with a buddy?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *