Kwa Sheria mpya ya Watoto na miongozo, serikali inadokeza kwamba familia ni mazingira ya malezi na ya kujali na ni mahali pazuri pa kumlea mtoto.
Hivi sasa kuna usitishaji wa usajili wa taasisi mpya na Sheria ya Mtoto, 2022 inayotoa kipaumbele kwa matunzo mbadala ya kifamilia, tofauti na kukuzwa kwa watoto katika Makazi ya Watoto.
Akizungumza katika Kaunti Ndogo ya Kiambu wakati wa kuunda Kamati ya Marekebisho ya Huduma. Mshirikishi wa Watoto wa Kaunti ya Kiambu (CCC) Bi Rose Mbarine alisema kuwa, ingawa taasisi za watoto zimekuwa zikifanya kazi nzuri, ni wakati wa nchi kuhamia kwa malezi ya nyumbani.
Alifafanua kuwa katika hali nyingi masuala ya umaskini, kutelekezwa na kutowajibika kwa wazazi ni sababu kubwa ya watoto kuishi katika taasisi hizo, lakini yote hayo yanaweza kushughulikiwa iwapo wadau wote wanaweza kushirikiana na kuwapa watoto mazingira mazuri ya kustawi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kamati hiyo, Hakimu Mkuu wa Mahakama ya Watoto ya Kiambu Manuela Kinyanjui alisema kama idara ya mahakama wanakumbatia mageuzi ya malezi na kwamba ni wakati wa wadau wote wanaohusika kuhudumia masilahi ya mtoto.
Peter Kamau kutoka Child in Family Focus alisema kazi yao ni utetezi katika kusaidia nyumba za watoto juu ya malezi ya nyumbani kama chaguo mbadala zaidi ya kuanzishwa kwa taasisi.
Kamau alieleza kuwa mageuzi ya malezi ni mchakato wa mabadiliko na haitakuwa jambo la siku moja, huku akiongezea kusema kuwa, Sheria mpya ya Mtoto ambayo ilizinduliwa rasmi Juni inapendekeza kwamba kamati za marekebisho ya malezi ziundwe katika kila kaunti na Kaunti Ndogo ili kusaidia kuongoza na kusimamia utekelezaji wa matunzo mbadala ya familia.
Kenya inakadiriwa kuwa na watoto milioni 3.6 ambao ni mayatima na walioainishwa kama walio katika mazingira magumu. Kati ya watoto hao 646,887 ni yatima wa wazazi wote wawili na takriban watoto 45,000 wanaishi katika taasisi zaidi ya 800 za misaada nchini.
Sheria hiyo mpya kuhusu watoto ilitiwa saini na Rais Uhuru Kenyatta na kuanza kutekelezwa Julai mwaka huu.
Aidha kwa mujibu wa UNICEF, watoto wanaoishi katika taasisi mara kwa mara wanatengwa na familia zao na jumuiya za mitaa, wananyimwa matunzo ya wazazi na kuvumilia madhara ya kimwili, kisaikolojia, kihisia na kijamii, na matokeo ambayo hudumu maisha yote.
Pia wana uwezekano mkubwa wa kukumbwa na ukatili, unyanyasaji, kutelekezwa, na unyonyaji.
Ilhali Ushahidi unaonyesha kwamba watoto hustawi zaidi wanapozungukwa na matunzo thabiti, ya malezi, upendo na ulinzi kutoka kwa wazazi na walezi.
Hii hutoa msingi unaohitajika ili kukuza ustawi muhimu, wa maisha marefu ya kiakili, kijamii na kimwili.
Utafiti unaonyesha kwamba, watoto wengi wanaoishi katika taasisi nchini Kenya wana mzazi aliye hai, na wengi ambao hawana, wana familia kubwa, ambao wangeweza kutoa malezi ikiwa wangekuwa na rasilimali na usaidizi wa kufanya hivyo.
Watoto wanawekwa kwenye taasisi hasa kwa sababu ya umaskini na ukosefu wa huduma za msingi kama vile chakula, makazi bora, matibabu, elimu, na matunzo maalumu kwa watoto wenye ulemavu.
Leave a Reply