mtoto.news

Ongezeko la kesi za utumizi wa dawa za kulevya miongoni mwa watoto

October 3, 2022

Matumizi mabaya ya dawa za kulevya ni suala zito linaloathiri sehemu zote za jamii, bila kujali umri, elimu au hali ya kiuchumi.

Inasikitisha sana kuona kwamba kila kukicha kunakuwa na taarifa za kukamatwa kwa wauza dawa za kulevya katika nchini Kenya.

Katika mahojiano na Afisa wa Marekebisho ya Gucha, Elijah Omanga, Kenya News Agency,  ilibaini kuwa kuna ongezeko la mara kwa mara la visa vya utumizi wa dawa za kulevya miongoni mwa watoto wanaosoma shule katika eneo la Kisii.

Kulingana na rekodi zilizothibitishwa na Omanga, kati ya kesi 200 katika Mahakama za Sheria za Gucha kati ya Januari na Septemba mwaka huu, 98 zilikuwa kesi za matumizi ya dawa za kulevya, ambayo ni takriban nusu ya takwimu hizo.

Katika kipindi hicho, vijana 77 walio na umri wa kati ya miaka 14 na 17 kutoka eneo hilo wamewekwa kwenye majaribio katika juhudi za kuwarekebisha kutoka kwa uraibu wa dawa za kulevya.

Halikadhalika, imekuwa tatizo kubwa kwa elimu ya watoto na maisha yao, huku ikiendelea kuwaangamiza watoto wengi  katika jamii.

Omanga anaeleza zaidi kuwa dawa hizo, hasa bangi, zinasambazwa kutoka maeneo ya mbali kwa kutumia pikipiki na wakati mwingine magari.

Omanga anasema kwamba, wachuuzi hao husambaza dawa hizo kwa mawakala katika eneo hilo ambao huwauzia vijana kwa haraka.

Baadhi ya watoto hao hasa wa kiume wameshirikishwa kusaidia kusambaza dawa hizo.

Omanga hata hivyo anabainisha kuwa maeneo ambayo madawa hayo yanasambazwa yanaweza kutambuliwa kwa urahisi.

Kando na bangi, kuna ongezeko la unywaji wa chang’aa katika eneo hilo ambalo pia limepuuza juhudi za kujaribu kuwakomboa watoto hao kutokana na utumizi wa dawa za kulevya.

Wasiwasi ni kwamba ni wazazi wa watoto wale wale wanaoshiriki katika utayarishaji wa pombe.

Zaidi ya kuwa na sheria na sera zilizoundwa ili kudhibiti matumizi mabaya ya dawa na kanuni kwa waraibu wa dawa za kulevya, ni jukumu la kila mtu katika jamii kuleta mabadiliko au matokeo yanayotarajiwa katika jamii zetu.

Kabla hatujachelewa, sote tunapaswa kuzingatia kwa makini hatari hii kubwa.

Serikali inafaa kuzingatia kupunguza matumizi mabaya ya aina tofauti za dawa na pombe ili kuhakikisha kuwa hatua madhubuti za usalama zimechukuliwa.

Katika ngazi za kijamii na kibinafsi, lazima tuchangie kwa nguvu katika kuangamiza suala hili.

Aidha, ni wajibu mkubwa kwa wazazi kutangamana na watoto wao na kutengeneza akili zao katika mwelekeo wenye tija na kuwafanya wajishughulishe na kazi zenye manufaa kwao na jamii kwa ujumla.

Omanga anaamini kuwa udhibiti wa wazazi ikiwa ni pamoja na hali ya afya ya nyumbani ni mojawapo ya zana bora katika kukabiliana na tishio la uraibu wa dawa za kulevya kwa watoto.

Hey, like this? Why not share it with a buddy?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *