Wakati kikundi kazi cha wanachama 49 kinajadili jinsi ya kurekebisha sekta ya elimu kwa mtaala unaozingatia umahiri kama kazi yake ya kwanza, walimu na wanafunzi katika maeneo ya mbali yaliyokumbwa na ukame wanatatizika kuendana na majukumu mapya kulingana na mtaala.
Lakini kazi hizo ni kidokezo tu kwani ukosefu wa vyumba vya madarasa umefanya mchakato wa elimu kwa baadhi ya walimu na wanafunzi kuwa na mtafaruku!
Hassan Bora, mwalimu kutoka shule ya msingi ya Kavunzoni anasema kwamba, Kwa sasa wanafunzi wa daraja la kwanza na la pili wanalazimika kubanana ndani ya darasa moja, hii ikileta utatanishi na ukosefu wa kuzingatia darasani kwa wanafunzi hao kwani wanasoma mosomo tofauti kwa wakati mmoja.
Isitoshe, walimu wanalazimika kuweka hema makazi yao kwenye madarasa ya wanafunzi hao. Walimu wawili wanalazimika kutumia dawati moja, kwenye darasa moja, ambalo wanafunzi wa daraja la kwanza na la pili wanasoma pamoja kwa wakati mmoja.
Aidha, eneo hili pia linakumbwa na ukame wa kupita mipaka, na hivyo somo la upandaji miti linakuwa na kusikitisha na la kukata tamaa kabisa, kwani watoto hawa wanajitahidi kupanda miti ila mbegu zinakauka, na mimea inadumaa.
Watoto kadhaa wanajaribu kuleta maji shuleni ili kunyunyizia kwa mimea hiyo, ila hali hiyo ni ngumu mno kwani kuna uhaba mkuu wa maji mjini Ganze. Watoto hawana maji ya kunywa, sembuse maji ya kunyunyizia miche?
Watoto wengi wamewacha shule na kuanza kufanya kazi za vibarua kama vile, uchomaji wa makaa na kufanya bodaboda ili kuwasaidia wazazi wao kumudu mahitaji ya kimsingi.
Mtaala wa CBC unahitaji fedha ili kununua bidhaa zinazohitajika shuleni, ila wazazi wana uhaba wa pesa kutokana na ukame uliokakamaa. Na iwapi mzazi atapata pesa, basi la kwanza atakalofikiria ni tumbo la mtoto wake na sio bidhaa za CBC.
Leave a Reply