UNICEF imeonya kwamba, ukosefu wa mvua nchini Kenya kumewasababisha watoto wapatao milioni 1.4 kukosa chakula chenye lishe bora, na maji safi ya kunywa.
Watoto hao pia wanakosa elimu, huduma za afya na ulinzi dhidi ya ukatili na kutelekezwa. Turkana ni miongoni mwa kaunti 15 zilizokumbwa na ukame nchini Kenya kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa na athari zinazoendelea za Covid-19, ambapo karibu mtoto mmoja kati ya watatu anaugua utapiamlo.
“Katika Pembe ya Afrika watoto wanakufa kwa njaa huku mamilioni wakiwa ukingoni mwa njaa hivi sasa,” Balozi wa Ukarimu wa UNICEF, mwigizaji Priyanka Chopra Jonas alisema na kuongeza kuwa “hivi ndivyo mabadiliko ya hali ya hewa yanavyoonekana hapa” na aliahidi kwamba, UNICEF itasambaza “vyakula vya matibabu vilivyojaa virutubishi ambavyo vinaweza kuokoa maisha ya mtoto.”
Kaimu Mwakilishi wa UNICEF Kenya, Jean Lokenga alisema kwamba, “hali mbaya inaweza kuwa mbaya zaidi, haswa ikiwa msimu ujao wa mvua hautatokea au iwapo bidhaa za kuokoa maisha kama vile chakula cha matibabu kilicho tayari kutumika (RUTF) kukosa kupatikana kwa sababu ya uhaba wa fedha.”
Kulingana na ripoti ya Septemba ya Mamlaka ya Kitaifa ya Kudhibiti Ukame (NDMA), angalau kaunti 10 ziko katika awamu ya hatari ya ukame, 10 katika awamu ya ukame, na tatu ziko katika awamu ya kawaida ya ukame kutokana na msimu wa wastani.
Ripoti hiyo ilibainisha kuwa watoto 942,000 walio chini ya miaka mitano wanahitaji matibabu ya utapiamlo mkali ikilinganishwa na 884,454 mwezi Agosti.
Pia, wanawake wajawazito na wanaonyonyesha 134,000 wanahitaji matibabu ya utapiamlo mkali ikilinganishwa na 115,725 mwezi Agosti.
Katika kukabiliana na hali hiyo, UNICEF inaongeza huduma za lishe na kusambaza maziwa ya matibabu na RUTF kwa vituo vya afya kando na kusaidia serikali kutambua na kutibu watoto wenye utapiamlo katika maeneo magumu kufikiwa.
“Ukweli nchini Kenya ni kwamba watoto wengi hawapati matibabu wanayohitaji, na wako katika hatari ya kipekee. Watoto ambao kinga zao tayari zimedhoofika kutokana na utapiamlo hawawezi kupigana na magonjwa, ikimaanisha kuwa wana uwezekano wa kufa kwa ugonjwa sawa na njaa,” alisema Chopra na kuongeza kuwa alikutana na jamii ya Kijiji cha Sopel ambacho wanachama wake wamehama kutafuta maji. na malisho kwa sababu ya ukame katikati mwa Turkana.
Jumuiya ya Sopel, hata hivyo, ilipata kisima kinachotumia nishati ya jua kwa matumizi ya nyumbani na kwa ajili ya matumizi ya zahanati ya eneo hilo na shule ya msingi kutoka UNICEF ambayo pia ilitoa vifaa vya dharura vya WASH kwa familia zilizoathiriwa na ukame kutibu maji nyumbani.
Familia zilizo katika mazingira magumu pia zilipokea uhamisho wa fedha ili kusaidia na gharama za afya na kulinda watoto kutokana na ndoa za utotoni na kuacha shule.
Leave a Reply