mtoto.news

Samburu Yaongoza kwa Idadi ya Mimba za Utotoni: Ripoti ya KDHS 2022

January 17, 2023

Ripoti ya KDHS 2022

Kulingana na ripoti ya KDHS iliyotolewa leo, Kaunti ya Samburu inaongoza na asilimia 50 ya mimba za utotoni, huku Kaunti ya Nyeri na Nyandarua ikiwa na asilimia 5.

Ripoti hiyo iliyofanywa na Utafiti wa Idadi ya Watu na Afya Nchini Kenya(KDHS),  kuanzia Februari 17 hadi Julai 13, 2022, ilihusisha takriban kaya 37,911. Ripoti hiyo imeangazia sehemu tofauti tofauti ikiwa ni pamoja na viwango vya uzazi, mimba za utotoni, chanjo na  magonjwa ya utotoni na ukeketaji miongoni mwa mengine.

Lengo kuu la Ripoti hiyo ni kutoa makadirio ya kisasa ya viashiria vya kijamii na kiuchumi pamoja na idadi ya watu, afya na lishe ili kuongoza upangaji, pamoja na utekelezaji, ufuatiliaji na tathmini ya idadi ya watu, afya na lishe katika ngazi ya kitaifa na kaunti kwa ujumla.

Aidha, Ripoti hiyo iliweza kuonyesha kwamba, kwa watoto walio na miaka 15 hadi 19 kuna asilimia kubwa zaidi ya mimba za utotoni kutoka kwa wale ambao hawajasoma,kuliko  kwa waliosoma zaidi.

Takriban wanawake 4 kati ya 10 wenye umri wa miaka 15-19 ambao hawajasoma wamewahi kupata mimba, ikilinganishwa na
ni asilimia 5 tu ya wanawake ambao wana kiwango cha elimu zaidi ya sekondari.

Vile vile vijana wa kike walio katika kiwango cha umaskini wana uwezekano mkubwa wa kuwa wajawazito kuliko wanawake walio katika kiwango cha juu cha utajiri.

Isitoshe, kiwango cha asilimia ya mimba za utotoni kati ya Kaunti zote nchini Kenya inatangulizwa na Kaunti ya Samburu iliyo na asilimia 50, huku West Pokot ikiwa na asilimia 36, Marsabit ikiwa na asilimia 29, Narok ikiwa na asilimia 28 na Meru ikiwa na asilimia 24.

 

Hata hivyo, ripoti hiyo imeonyesha upungufu wa kiwango cha uzazi nchini kenya kutoka asilimia 3.9 mwaka wa 2014 hadi asilimia 3.4 mwaka wa 2022.

Uwezo wa uzazi ni mdogo miongoni mwa vijana ambapo kuna uwezekano wa wazazi 73 kwa kila wanawake 1,000 wenye umri wa miaka 15 hadi 19, huku kilele cha uzazi ni 179 kwa kila 1,000 kati ya wanawake wenye umri wa miaka 20-24.

Asilimia 15 ya wanawake wenye umri wa miaka 15-19 wamewahi kuwa wajawazito, huku asilimia 12 wakijifungua watoto walio hai, ilihali asilimia 1 wakipoteza watoto wao kabla au wakati wa kujifungua.

Asilimia ya wanawake wenye umri wa miaka 15-19 ambao wamewahi kupata mimba huongezeka kadiri umri unavyoongezeka, kutoka asilimia 3 kati ya wale wenye umri wa miaka 15 hadi asilimia 31 kati ya wale wenye umri wa miaka 19.

 

 

 

 

 

Hey, like this? Why not share it with a buddy?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *