mtoto.news

Watoto wanalia njaa huku viwango vya utapiamlo vinaongezeka

January 26, 2023

Kambi ya Dadaab. Paul Odongo/MSF

Shirika la misaada la MSF limeripoti ongezeko la asilimia 33 ya wagonjwa wenye utapiamlo katika eneo kubwa la Dadaab baada ya watu kufurika kutoka Somalia iliyokumbwa na ukame.

Utapiamlo miongoni mwa watoto umeongezeka, hasa katika mojawapo ya kambi kubwa zaidi za wakimbizi duniani mwaka uliopita huku wasiwasi ukiongezeka kutokana na hali mbaya zaidi katika eneo hilo nchini Kenya. Ndani ya mwaka mmoja (2022) Shirika la Médecins Sans Frontières (MSF)liliweza kutibu wagonjwa asilimia 33 wakiwemo watoto kutokana na utapiamlo, huku shirika hilo likisisitiza kwamba, kwa sasa maisha katika kambi hiyo ni magumu mno.

Dadaab, iliyo kaskazini mwa Kenya, ilifunguliwa mwaka 1991 kama eneo la kupita kwa wakimbizi wanaokimbia vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Somalia. Hata hivyo, kutokana na mzozo wa muda mrefu katika Pembe ya Afrika na janga la njaa katika kanda hiyo, kufikia Septemba Dadaab ilikuwa makazi ya zaidi ya wakimbizi 233,000, hii ni zaidi ya mara tatu ya idadi iliyokusudiwa kuhudumia. Idadi ya waliowasili inakadiriwa kuongezeka kwa zaidi ya 100,000 kufikia Aprili.

Mashirika ya misaada ya kibinadamu yanasema kwamba, kufurika kwa wakimbizi wapya kumeathiri rasilimali za chakula na maji na vyoo. MSF, ambayo imefanya kazi huko Dadaab kwa karibu miongo mitatu, inaonya kwamba ongezeko hilo linaweza kuongeza mzozo ambao mashirika ya kibinadamu hayataweza kudhibiti. Takriban familia 800 kwa sasa zinaishi nje ya eneo la Dadaab bila kupata huduma za kimsingi.

MSF pia imeibua wasiwasi juu ya kuongezeka kwa visa vya kipindupindu katika kambi hiyo na kaskazini mwa Kenya , ikiwa ni pamoja na Garissa na Wajir. Kulingana na MSF tangu kuzuka kwa ugonjwa huo kutangazwa Oktoba, kesi 716 zimeripotiwa. Madaktari wanaripoti kwamba mlipuko huo umechukua muda mrefu zaidi kuliko milipuko midogo ya mara kwa mara ambayo kambi imepata katika miaka ya hivi karibuni.

Maeneo ya kaskazini mwa Kenya na Somalia yameathiriwa sana na ukame mbaya zaidi , ukame ambao haujawahi kukumba Afrika Mashariki katika kipindi cha miaka 40. Mkoa huo unajiandaa na msimu wake wa sita mfululizo wa ukosefu wa mvua mwaka huu. Mamilioni ya watu wanakabiliwa na njaa na ufukara.

Mashirika ya misaada ya kibinadamu yanasema kwamba, yana wasiwasi kuhusu jinsi yatakavyoweza kukidhi mahitaji ya watu katika kukabiliana na kupungua kwa ufadhili wa wakimbizi.

Hey, like this? Why not share it with a buddy?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *