Idara ya Jimbo la Huduma za Urekebishaji na Idara ya Mahakama zimeanza kushughulikia kuondoa msongamano magerezani hasa katika mchakato unaolenga wakosaji wa uhalifu mdogo mdogo, pamoja na akina mama.
Katibu Mkuu katika Idara hiyo Mary Muthoni, alifanya ziara ya ghafla hapo Jumatatu katika Gereza la Nakuru ambapo alisema kwamba, hatua hiyo ililenga kupunguza mateso ya watoto wa wafungwa hao.
“Suala la watoto wadogo wasio na hatia katika magereza yetu linagusa sana. Tunashirikiana na Idara ya Mahakama kuhakiki kesi za mama zao,” alisema Muthoni. Alieleza kuwa kuwaweka watoto gerezani kunaathiri maendeleo yao. “Kufikia Januari 30, tulikuwa na watoto kumi katika Gereza la Wanawake la Nakuru. Katika vituo vote nchini, kuna takriban watoto 300 walio chini ya umri wa miaka minne. Hii ni idadi kubwa mno,” alisema.
Aidha Muthoni alieleza kuwa idara hiyo inashirikiana kwa karibu na Mahakama kuhakikisha kina mama waliofungwa kwa makosa madogo na watoto wao wanaachiliwa. “Baadhi ya akina mama hawakufanya makosa ya kifo ambayo yanaweza kuwaweka gerezani kwa muda mrefu. Ikiwa ni makosa madogo, tunawaacha waende na kuwapatia adhabu ya kufanya kazi za jamii,” aliongeza.
Aliongeza kuwa idara ya mahakama imejitolea kuhakikisha kuwa idadi ya watu waliofungwa jela na waliojitolea kurudi rumande inapungua. “Wahalifu wa mambo madogo madogo wanapaswa kurekebishwa kwa njia tofauti badala ya kuwafunga. Wale walioko rumande hawafai kuzuiliwa kwa muda mrefu kwani wanaweza kupatikana bila hatia miaka mingi baadaye,” alisema.
Aliongezea kusema kuwa ,hii inaendana na ajenda ya serikali ya kuhakikisha watu wote walio katika umri wa uzalishaji wanashiriki kikamilifu katika kusaidia katika ujenzi wa taifa. Muthoni alibainisha kuwa sababu ya kuwashikilia wahalifu katika vituo si kuwaadhiby bali ni kwa ajili ya kuwasahihisha. “Ikiwa mkosaji yuko gerezani, lengo kuu linafaa kuwa kuwapa ujuzi ambao utawasaidia kuendeleza maisha yao watakapoachiliwa,” Muthoni alisema.
Isitoshe, serikali inajitahidi kuimarisha njia mbadala za utoaji haki ili kuhakikisha makosa madogo madogo yanashughulikiwa kwa kiwango cha chini kabisa. “Baadhi ya kesi hizi ndogo ndogo zinaweza kusuluhishwa nje ya mahakama badala ya kuwashikilia watu wenye tija gerezani. Kila mtu anastahili nafasi ya pili. Tunataka kusahihisha watu katika ngazi ya chini kabisa, kuanzia wazee wa vijiji na machifu,” alisema Muthoni.
Muthoni alitaja maswala ya kifamilia ambayo yanaweza kutatuliwa nje ya mahakama ili kushughulikia msongamano usio wa lazima gerezani.
PS alisema kwamba, serikali pia inajitahidi kuboresha ustawi wa wafungwa na maaskari wa magereza kwa kuzingatia viwango vya Umoja wa Mataifa.
Leave a Reply