mtoto.news

Tetemeko la ardhi Uturuki/Syria;Watoto walioachwa yatima wanakabiliwa na mustakabali usio na uhakika

February 13, 2023

Ghaith Alsayed/AP

Kila mtoto ana haki ya kuwa na afya njema na kukuzwa katika mazingira salama na safi. Kila mtoto ana haki ya kuishi na kukua kwa njia bora zaidi, ila baada ya mtetemeko wa ardhi huko maeneo ya Uturuki na Syria watoto wengi wameachwa katikati ya ghasia, uharibifu na machafuko.

Aya alizaliwa chini ya vifusi vya tetemeko kuu la ardhi lililotokea hapo Jumatatu wiki iliyopita, akiwa bado ameambata kwenye maiti ya mama yake kupitia kamba ya kitovu wakati waokoaji walipompata. Cha kusikitisha ni kwamba mama wa mtoto huyo hakunusurika na inadhaniwa kuwa alifariki saa chache baada ya kujifungua. Binamu yake aliiambia shirika la habari kwamba, mtoto huyo anaaminika kuwa mwokozi pekee wa familia yake ya karibu.

Kwa sasa Aya anapokea matibabu katika hospitali ya watoto katika mji wa karibu wa Afrin, ambapo daktari wa watoto Hani Maarouf aliiambia AFP kwamba, mtoto yuko sawa ila alifikishwa hospitalini akiwa tayari na michubuko, majeraha na hypothermia.

Vile vile, Tariq Haidar mwenye umri wa miaka 3 alitolewa akiwa hai kutoka kwenye mabaki ya nyumba yao huko Jandaris, kaskazini mwa Syria, shirika la habari la Reuters liliripoti kwamba, Tariq Alipelekwa hospitalini ambapo madaktari walilazimika kukata mguu wake wa kushoto.

Familia yake haikunusurika. Malek Qasida, muuguzi anayemhudumia, aliiambia Reuters kuwa, “Walimtoa baba yake na ndugu zake wawili mbele yake, wakiwa tayari wamefariki.” Mwili wa mamake na ndugu wa tatu ulipatikana baadaye kutoka kwenye mabaki hayo, wenyeji walisema.

Aya na Tariq ni watoto wawili tu kati ya idadi isiyojulikana ya watoto nchini Uturuki na Syria ambao wameachwa yatima kufuatia tetemeko kubwa la ardhi.

“Ingawa bado hatuna idadi yoyote iliyothibitishwa, kwa kuzingatia janga kubwa, na kuongezeka kwa idadi ya vifo, ni wazi kwamba watoto wengi watakuwa wamepoteza wazazi au walezi katika tetemeko hili,” UNICEF ilinena

“Kutambua kwa haraka watoto wasio na walezi na wale ambao wanaweza kuwa wametenganishwa na wazazi na walezi ni jambo la msingi kabisa ili waweze kupata matunzo na usaidizi stahiki kwa muda mfupi, na ili tuanze kazi ya kuwatafuta na kuwaunganisha na familia.

“Kufuatia majanga ya aina hii, watoto waliokimbia makazi yao, hasa wale ambao hawajasindikizwa au kutengwa na familia, wako katika hatari ya kudhulumiwa, kunyonywa na kunyanyaswa, ikiwa ni pamoja na hatari ya biashara haramu ya binadamu au unyanyasaji wa kijinsia.

Taarifa kuhusu idadi kamili ya watoto walioachwa bila wazazi bado haijafahamika. Kulingana na Wizara ya Familia na Huduma za Jamii ya Uturuki siku ya Ijumaa, familia za watoto 263 ambao walitolewa kutoka kwa vifusi nchini Uturuki hazikuweza kufikiwa.

Kati ya watoto hao, 162 wanaendelea kupatiwa huduma hospitalini, huku watoto 101 wakihamishwa katika vitengo husika vya wizara na kupelekwa chini ya uangalizi wa kitaasisi baada ya matibabu yao.

Kulingana na mamlaka, idadi ya vifo nchini Uturuki na Syria inafikia zaidi ya 28,000.

Hey, like this? Why not share it with a buddy?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *