Wazazi katika Kaunti ya Pokot Magharibi wameonywa dhidi ya kukwepa majukumu yao ya uzazi, na kuhimizwa kutanguliza elimu ili kukuza vizazi vya kesho.
Kamishna Msaidizi wa Kaunti ya Tapach (ACC) Ibrahim Masiaga alibainisha kuwa, ofisi yake imekuwa ikishughulikia visa vingi vya utelekezaji wa watoto, haswa katika suala la watoto wale waliokusudiwa kuvuka kidato cha kwanza kwani wazazi wengi hupuuza jukumu lao la kulipa karo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa jumba la kisasa la kulia chakula katika shule ya msingi ya kutwa ya Amani ya Kamelei na Shule ya Msingi ya Bweni ya Kamelei katika Kaunti Ndogo ya Pokot Kusini mnamo Jumatano. Masiaga alinena kuwa, utawala wake hautaunga mkono visa vyovyote vya wazazi kurushiana majukumu wakati wa visa vya utelekezwaji wa elimu ya watoto.
“Hatutaruhusu wazazi kutupiana uwajibikaji katika masuala ya elimu ya watoto wao. Na Iwapo kutakuwa na tofauti za ndoa, basi mtoto hafai kuwa mtu wa kutolewa kafara,” ilishinikiza ACC.
“Serikali ina wasiwasi kuhusu baadhi ya wazazi kukataa kuwalipia karo watoto wao wanapotaka kujiunga na shule ya upili ilhali wana uwezo wa kufanya hivyo,” ACC alisikitika.
Aliteta kuwa, Kaunti ya Pokot Magharibi ilikuwa na bahati kwa sababu washikadau mbalimbali wameungana kusaidia wazazi kukidhi karo za shule kupitia utoaji wa karo za serikali ya kaunti, hazina ya Kitaifa ya Maendeleo ya Maeneo Bunge (NG-CDF) miongoni mwa zingine huku wazazi wakiachwa na pesa kidogo za kulipa kutoka mifukoni mwao.
Alibaini kuwa, eneo hilo likiwa kwenye mpaka wa kaunti za Pokot Magharibi na Elgeyo Marakwet, basi imekuwa mtindo kwa baadhi ya wazazi kuhamia ng’ambo ya pili watoto wanapodai karo ili kujiunga na shule ya upili.
Msimamizi huyo alilaani wazazi hao ambao walionyesha kusitasita juu ya ustawi wa elimu ya watoto wao hasa wale waliozaliwa nje ya ndoa, huku akibainisha kuwa kila mmoja wa wazazi hao wawili lazima atimize wajibu wake katika kuhakikisha watoto hao wanapata haki yao ya elimu bila kubaguliwa.
Masiaga alisikitika zaidi kwamba baadhi ya wazazi wanakwepa kuuza mifugo yao ili kuwalipia ada watoto wao. “Tunajua nyakati zinaweza kuwa na changamoto lakini kama una mifugo kwa nini usitumie uwekezaji huo ili kuwapeleka watoto wako shuleni?” alishangaa ACC huku akitoa wito kwa wazazi kutekeleza jukumu lao katika kusaidia usimamizi wa shule kutoa mazingira bora ya kujifunzia kupitia kulipa ada kwa wakati.
Wakati huo huo, Masiaga amewashauri wakazi kukumbatia upangaji wa uzazi ili waweze kulea familia ambazo wanaweza kuzisimamia bila dhiki. Alikariri kuwa kuwawezesha watoto kupitia elimu kutasaidia katika kushughulikia migogoro ya kifamilia ambayo kwa kawaida hutokana na mzozo wa rasilimali za ardhi ya familia.
Leave a Reply