mtoto.news

Beatrice Mwende; Aliyewaua Watoto Wake Wanne Ahukumiwa Kifungo cha Maisha

March 2, 2023

 

 

Beatrice Mwende, Mwalimu wa Hisabati anayeishi Naivasha, Ahukumiwa kifunga cha maisha baada ya Kuwaua wanawe wanne.

Beatrice Mwende, mwalimu wa Hisabati anayeishi Naivasha ambaye aliwaua watoto wake wanne mnamo Juni 2020, atatumikia kifungo cha maisha jela kwa mauaji hayo. Jaji wa Mahakama Kuu ya Naivasha Grace Nzioka alipuuzilia mbali utetezi wa Mwende kwamba alikuwa na mapepo alipowaua binti zake watatu na mwanawe mmoja.

Beatrice Mwende

Mfungwa huyo mwenye umri wa miaka 44 hapo awali alikana mashtaka, lakini baadaye, mwaka wa 2022, alikiri kuwaua watoto wake. Alisema kwamba, alibadili mawazo yake baada ya kushauriana na wakili wake. Waliouawa ni Melody Warigia (miaka 8), Willy Macharia (miaka 6), Samantha Njeri (miaka 4) na Whitney Nyambura (miaka 2).

Mwende aliwanyonga wanne hao nyumbani kwake Kabati Estate huko Naivasha mnamo Juni 26, 2020. Jaji Nzioka, alipokuwa akitoa uamuzi huo mnamo Alhamisi, Machi tarehe 2, alisema kuwa, uchunguzi wa kiakili uliofanywa kwa Mwende ulionyesha kuwa alikuwa na akili timamu alipotenda makosa hayo. Mfungwa huyo aliiambia mahakama kwamba katika tarehe ambayo aliwaua watoto wake, alikuwa “amepagawa na pepo wachafu”.

“Kisingizio chake cha kupagawa na baadhi ya pepo wachafu wakati anafanya kitendo hicho, hakiwezi kuthibitishwa mahakamani. Kwa hivyo, amehukumiwa kifungo cha maisha jela,” akaamua Jaji Grace Nzioka. Aidha, hakimu huyo alinena kwamba, uhalifu wa Mwende unavutia kifungo cha maisha jela kwa kila moja ya mauaji manne.

Hata hivyo, Hakimu Nzioka alisema kwa kuwa shtaka la kwanza lilikuwa tayari limemhukumu kifungo cha maisha jela, atatumia muda gerezani chini ya hukumu ya kwanza. Jambo la kushangaza ni kwamba Mwende alikuwa akitabasamu wakati wa uamuzi huo. Ana siku 14 za kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo.

Mwendesha mashtaka Nelly Maingi aliambia mahakama kwamba mnamo Juni, tarehe 26, 2020, Mwende alianza kwa kumnyonga mtoto wake mdogo, Whitney Nyambura, 2, kabla ya kuendelea na mauaji ya watatu waliosalia. Yeye, baadaye, alilala katika nyumba hiyo hiyo na akakimbia asubuhi iliyofuata (Juni 27, 2020). Asubuhi hiyo, aliwapigia simu jamaa zake na kuwafahamisha kwamba amewaua watoto wake, na alikuwa anawaomba (jamaa zao) msamaha.

Mwendesha mashtaka aliambia mahakama kuwa Mwende alikamatwa baadaye Juni 27, 2020 katika nyumba ya kulala wageni huko Kayole Estate, Kaunti Ndogo ya Naivasha. “Ripoti ya uchunguzi wa maiti ilionyesha kuwa watoto hao walikufa kutokana na kunyongwa koo,” mwendesha mashtaka Nelly Maingi aliambia mahakama.

Hey, like this? Why not share it with a buddy?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *