mtoto.news

Zaidi Ya Wanafunzi 4,000 Wapokea Ufadhili Uliosalia Sh. Milioni 25.5

March 13, 2023

Pic@UN

Zaidi ya wanafunzi 4,000 kutoka eneo bunge la Isiolo Kaskazini watapokea Sh. milioni 25.5 kama ufadhili katika jitihada za kuhakikisha kwamba wanafunzi wanasalia shuleni licha ya ukame unaoshuhudiwa na gharama kubwa ya maisha nchini.


 

 

Kulingana na Mbunge wa Isiolo Kaskazini Bw Joseph Samal ambaye amezindua Sh. Milioni 25.5 za ufadhili zitakazowanufaisha wanafunzi 4,326 kutoka jimboni kwake na kuongeza kuwa serikali imejipanga kuhakikisha wanafunzi wote wanatendewa kwa usawa katika kutoa fursa za elimu bila kujali mikoa wanayotoka.

“Hakuna mwanafunzi atakayebaguliwa wakati wa kugawa ufadhili huu wa elimu, ingawa familia zilizo hatarini sana zitapata faida kwa sababu hazina chanzo kingine cha kutegemewa cha riziki,” mbunge huyo alisema.

Bw. Samal aliongezea kunena kwamba, Sh. milioni 24.5 zitawekwa katika maendeleo ya taasisi za elimu katika jimbo hilo pamoja na Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (TVET).

Aliwataka wakuu wote wa shule za upili kuwaruhusu wanafunzi wote kuendelea na masomo huku akisema kwamba, fedha zinazotolewa kupitia Hazina ya Kitaifa ya Maendeleo ya Maeneo Bunge (NG-CDF), pamoja na  idara ya Watoto, afisi ya serikali ya kaunti na mwakilishi wa wanawake zilitosha kwa kila mtoto katika kaunti hiyo.

“Wazazi ambao bado wanawaweka wanafunzi nyumbani kwa sababu ya matatizo ya karo wanapaswa kuwarejesha shuleni mara moja kwani ninatoa wito kwa wakuu wa shule kuhakikisha kuwa, hakuna mwanafunzi anayerudishwa nyumbani kwa sababu ya ukosefu wa karo,” alisema mbunge huyo.

Bw. Samal aliongezea kuwa serikali ya kitaifa ilikuwa ikishughulikia hali ya ukame inayotisha nchini kupitia msaada wa Sh. bilioni 16 kutoka USAID na nyongeza ya Sh.4 bilioni kutoka kwa washirika wengine.

Pia alifichua kuwa ‘World Vision’, shirika lisilo la kiserikali linalofanya kazi katika kaunti hiyo lilisaidia watoto 240 kwa ufadhili wa elimu kamili huku ‘Equity Bank’ ikiwapa baadhi ya watoto 600 ufadhili kamili hadi ngazi ya chuo kikuu.

Kamishna wa Kaunti ya Isiolo Bw. Geoffrey Omoding aliwaagiza Manaibu Kamishna watatu wa Kaunti kutoka eneo hilo kuhamasisha wananchi kupitia kampeni ya serikali ili kufikia kiwango cha lazima cha mpito cha asilimia 100 kwa wanafunzi wanaojiunga na Kidato cha Kwanza na wale wanaokwenda Sekondari ya Vijana.

Msimamizi huyo alisema kuwa, shule zote 81 za umma za JSS katika kaunti hiyo zimeanza na masomo yanaendelea licha ya uhaba wa walimu katika eneo hilo. Aidha, Kuhusu usalama, Bw Omoding alisema kuwa kaunti hiyo ina maafisa wa usalama wa kutosha na kuongeza kuwa serikali imefunga maeneo yote ambayo yalikuwa yakitumiwa na wahalifu hao hapo awali katika juhudi za kutokomeza vitendo vya wizi vinavyosumbua eneo hilo.

Hata hivyo, mkuu huyo aliongeza kusema kuwa serikali imesambaza chakula cha msaada cha kutosha kwa shule zote za sekondari na msingi za umma.

Hey, like this? Why not share it with a buddy?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *