Maji ni uhai, vile vile maji ni jambo muhimu mno katika maisha ya binadamu, Usafi wa mazingira na usafi kwa ujumla huzuia ueneaji wa magonjwa na maambukizi mbali mbali. Na iwapo maji yatakosekana, basi mahitaji mengi ya kimsingi pia yatakosekana. Watoto wengi hufa kutokana na ugonjwa wa kuhara, elimu yao huvurugika au kukwama, na utapiamlo huzidi kwa sababu ya kuongezeka kwa ukosefu wa chakula chenye afya na chakula cha kutosha huku ukosefu wa maji unaongeza changamoto za rasilimali kwani familia nyingi hulazimika kuhama na migogoro ya silaha huongezeka pamoja na ajira ya watoto.
Ripoti ya hivi majuzi ya UNICEF yasema kwamba, Maji yasiyo salama na usafi kwa ujumla unaendelea kusababisha magonjwa na vifo vinavyoweza kuzuilika kabisa miongoni mwa watoto. Kila siku, karibia takriban watu 4,000 hufa kutokana na magonjwa yanayotokana na shida ya maji, usafi na vyoo, huku zaidi ya vifo 1,000 ya vifo hivi ni miongoni mwa watoto walio chini ya miaka mitano.
Ulimwenguni, watoto milioni 600 bado hawana usalama wa maji ya kunywa, huku bilioni 1.1 wana ukosefu wa vyoo na milioni 689 wana ukosefu wa huduma ya msingi ya usafi. Isitoshe watoto milioni 149 bado wanakabiliwa na kulazimika kujisaidia haja kubwa kwa uwazi.
Ripoti hiyo imeeleza bayana kuwa kuna vipengele kadha wa kadha ambavyo vinachangia uwepo wa ukosefu wa maji, vyoo na hata usafi kwa ujumla.
La kwanza kabisa: Ongezeko la Idadi ya Watu na Uwepo wa Miji Mingi.
Iwapo idadi ya watu itaongezeka basi uchumi pia utakuwa, navyo viwango vya maisha vitapanda na mahitaji ya maji yataongezeka. Inakadiriwa kuwa, chini ya miaka kumi, miji 45 iliyo na takriban watu milioni 3 na zaidi itakuwa na uhaba mkubwa wa maji.
La Pili: Mabadiliko ya Anga.
Ukame unazidi kuongezeka, hasa kwenye jamii zilizo katika mazingira magumu, na iwapo kuna ukame, basi maji huwa kidogo mno, na hivyo migogoro husababishwa na desturi za usafi wa mazingira na vyoo hutupiliwa mbali. Vilevile, iwapo maji yatakosekana, nao watoto watashindwa kupata na kula chakula kilicho na afya na cha kutosha. Watoto na wanawake watalazimika kutembea kwa muda mrefu wakitafuta maji, jambo ambalo litawalazimu watoto kukatizwa masomo yao. Isitoshe kuongezeka kwa mawimbi ya joto na joto la juu sana
huongeza mahitaji ya maji na kiu kali.
Aidha, mafuriko husababisha uchafuzi wa maji, pamoja na mvua kubwa kutoka kwa dhoruba na vimbunga hueneza magonjwa kupitia wadudu wa maji.
La Tatu: Migogoro na Uhamaji
Ukosefu wa usalama wa maji ni sababu na athari ya migogoro na uhamiaji. Ukosefu wa upatikanaji wa maji unaweza kusababisha ushindani, mvutano na vurugu. Migogoro inayohusiana na maji imeorodheshwa kama wasiwasi mkubwa kwa hatari za kijamii. Iwapo kutakuwa na uhaba wa maji, basi familia zitalazimika kuhama. Na wakati watahamia jumuiya mpya, basi mahitaji ya maji yataongezeka na hivyo mivutano mipya itaundwa. Huu utakuwa mduara usio na mwisho.
Na hivyo, hatua muafaka na ya haraka inahitajika!
Leave a Reply