Mahakama ya Nairobi imeahirisha kesi ya wizi wa watoto dhidi ya Askofu Gilbert Juma Deya baada ya hakimu wa mahakama kusema alikuwa mgonjwa.
Deya, ambaye alifika mbele ya hakimu mkuu mwandamizi wa Milimani Robison Ondieki hapo jana, alikuwa tayari kwa kusikilizwa na kujitetea pamoja na wakili wake John Swaka. Mwendesha mashtaka mkuu wa serikali Nicholas Mutuku alisema pia yuko tayari kumhoji mshtakiwa katika utetezi wake. Hata hivyo Hakimu alisema kuwa, hajisikii vizuri na hivyo akaomba kuahirisha kesi hiyo.
Hata hivyo, kesi hiyo iliahirishwa hadi Aprili tarehe 20. Katika kesi hiyo, Deya anashtakiwa kwa makosa matano ya kuiba watoto watano, wote wenye umri wa chini ya miaka 14, tukio lilotokea kati ya mwaka wa 2002 na mwaka wa 2004, katika mtaa wa Mountain View. Mwezi uliopita, mshtakiwa aliitaka mahakama kumwachilia huru kwa kukosa ushahidi.
Wakati akijitetea kutokana na madai hayo, mhubiri huyo ambaye Agosti 4, 2017 alifukuzwa nchini Kenya kutoka Uingereza kujibu mashtaka ya wizi wa watoto, alikana mashtaka yote matano, askofu huyo alikanusha kuwa alitoa maagizo yoyote kwa mtu yeyote kuwaweka watoto hao watano katika nyumba yake ya Mountain View jijini Nairobi.
Hakimu Robinson Ondieki aliambiwa mashtaka hayo yalikuwa mabaya na yanalenga kuharibu sifa yake kama “mtu wa Mungu”, huku akidai kwamba, wakati wa makosa hayo, alikuwa nchini Uingereza. “Mheshimiwa sijashughulikia cheti cha kuzaliwa kwa wanaodaiwa kuwa watoto na matokeo ya DNA hayakuonyesha kuwa watoto hao ni wangu,” Deya alisema. Alikanusha kuzuru idadi ya hospitali au zahanati na kushikilia kuwa hana uhusiano wowote na watoto hao watano.
Swaka alidai kuwa upande wa mashtaka uliwasilisha vielelezo ambavyo vilishindwa kuonyesha kwamba mteja wake alikuwa na makosa au alikuwa na hatia bila shaka yoyote. “Hakukuwa na ushahidi wowote unaoonyesha kosa lililowekwa dhidi ya mshtakiwa,” alisema wakili huyo na kuongeza kuwa upande wa mashtaka ulitegemea mashahidi ambao walishindwa kuonyesha kwamba Deya alipokea au kusafirisha watoto.
One reply on “Kesi ya Wizi wa Watoto Dhidi ya Deya imesogezwa hadi Aprili”
[…] aliye na utata nchini Kenya, ameondolewa mashtaka ya ulanguzi wa watoto kutokana na ukosefu wa ushahidi wa […]