Wadau wa elimu katika Kaunti ya Murang’a wamekutana ili kujadiliana kuhusu jinsi ya kupunguza Unyanyasaji wa Kijinsia (GBV) katika juhudi za kuimarisha ubora wa elimu.
Wakati wa mkutano wa uhamasishaji uliofanyika Jumatatu katika Shule ya Msingi ya Teknolojia mjini Murang’a, Mkurugenzi wa Elimu kaunti ndogo ya Murang’a Mashariki Samuel Ruitha alisema kuwa watoto wameathiriwa na GBV na hivyo, wazazi, walimu na jamii kwa ujumla wameonywa wajichunge dhidi ya tabia hii katika juhudi za kuinua ubora wa elimu katika kaunti hiyo.
Ukatili wa Kijinsia ni unyanyasaji unaoelekezwa kwa jinsia ya kibaolojia au utambulisho wa kijinsia wa mtu na hutokea katika aina mbalimbali, huku visa vingi vikiwa ni unyanyasaji wa kimwili na kingono.
Mkurugenzi huyo aliona kuwa unyanyasi wa kijinsia kwa watoto wanaokwenda shule husababisha ufaulu duni wa masomo, kuacha shule, ndoa za utotoni, utoro darasani miongoni mwa madhara mengine.
“Ni sera ya serikali kwamba tunapaswa kuwa na asilimia mia moja ya mabadiliko ya wanafunzi kutoka shule za msingi kwenda shule za sekondari au katika ngazi yoyote ya elimu,” alisema na kuongeza kuwa GBV ni moja ya sababu zinazoweza kuzuia mabadiliko haya na hata kusababisha idadi kubwa ya wahasiriwa kuteseka kwa iwapo hatua yeyote haitachukuliwa kwa haraka.
Bwana Ruitha alinena kwamba, Wizara ya Elimu kwa kushirikiana na Benki ya Dunia imekuja na mpango unaoitwa Mradi wa Kuboresha Ubora wa Elimu ya Sekondari (SEQUIP) unaolenga kuwawezesha wadau wa elimu kukabiliana na changamoto kama ukatili wa kijinsia unaoathiri ubora wa elimu.
“SEQUIP inalenga kuimarisha uhifadhi katika shule za msingi na mabadiliko kutoka elimu ya msingi hadi sekondari katika maeneo yaliyolengwa kupitia kuboresha miundombinu ya shule na utoaji wa ufadhili wa masomo, ushauri, utetezi, uhamasishaji wa jinsia na usaidizi wa kijamii,” alisema.
Kwa upande wake Naibu Kamishna wa Kaunti ya Murang’a Mashariki Thomas Nyoro amewashukuru washikadau hao kwa kujumuika kujadili masuala yanayosababisha GBV na athari zake katika ubora wa elimu.
“Ukatili wa kijinsia shuleni na majumbani unapaswa kuepukwa kwa gharama yoyote,” alisema, huku akiongezea kuwa, maovu hayo yanaathiri malezi ya watoto wetu kwa njia hasi na kusababisha wafanye vibaya shuleni pamoja na athari zingine.
Alisema kesi za unyanyasaji zinapaswa kuripotiwa mara moja kwa polisi na mamlaka nyingine zinazohusika kama vile Machifu.
Nakala kutoka KNA
Leave a Reply