Wanaharakati wa kutetea haki za watoto katika kaunti ya Bungoma wamewataka Magavana kutenga pesa kusaidia mipango ya watoto katika kaunti hiyo.
Akizungumza katika shule ya Xavarian Brothers’s kaunti ya Bungoma wakati wa kongamano la watoto David Lupao mwenyekiti wa shirika la kutetea haki za watoto kaunti ya Bungoma BCCRN amesema kuwa watoto wengi wanakumbwa na changamoto mbali mbali hivyo kuna haja ya serikali za kaunti kutenga rasilimali kusaidia programu za watoto.
Lupao alithibitisha kuwa Bunge la Watoto linawapa watoto mamlaka ya kuzungumza na kuripoti kesi za udhalilishaji kwa mamlaka husika ili zifanyiwe kazi. Alisema kuwa changamoto wanazopitia watoto ni pamoja na; ajira ya watoto, biashara ya watoto, ukeketaji, unajisi na unyanyasaji wa watoto. Lupao alisema kuwa BCCRN ni shirika la kijamii ambalo linapigania haki za watoto katika Kaunti ya Bungoma.
Lupao hata hivyo alitoa wito kwa wazazi na walezi kuwekeza katika mustakabali wa watoto wao, akibainisha kuwa Bungoma imekuwa katika rekodi mbaya kutokana na idadi kubwa ya mimba za utotoni na ukatili wa kijinsia. Aidha, Lupao alisema iwapo serikali za kaunti zitatenga fedha kwa ajili ya mipango ya watoto, inafaa kuboresha lishe, afya na elimu.
Nabakwe Naube, afisa wa watoto kaunti ya Bungoma alisema kuwa mkutano wa watoto hufanyika kote nchini shule zikifungwa. Aliongeza, kunena kuwa, baada ya siku tatu za kukutana na watoto, wao hutengeneza risala na kuiwasilisha kwa serikali za kaunti na kitaifa.
Nakala-the Star
Leave a Reply