mtoto.news

Takriban Watoto 6500 Hupotea Kila Mwaka Nchini Kenya

May 19, 2023

Hii ni sawa na watoto 18 kila siku.

Wakati ulimwengu unajiandaa kuadhimisha siku ya kimataifa ya watoto waliopotea, takwimu zimeonyesha kuwa, takriban watoto 6500 hupotea kila mwaka nchini Kenya, hii ni sawa na watoto 18 kila siku. Polisi wanasema kwamba, idadi hiyo inaweza kuwa kubwa zaidi ikizingatiwa kwamba watoto wengi zaidi waliopotea hawaripotiwi kamwe.

Polisi sasa wanawataka wananchi kuripoti watoto waliopotea ili kupata nyaraka zinazofaa.  Mkurugenzi Mtendaji na Mwanzilishi wa Missing Child Kenya Foundation Mary Munyendo alithibitisha kwamba wengi wa watoto walioripotiwa kupotea wangeweza kusafirishwa nje ya nchi. “Suala la kupotea kwa watoto ni tatizo nchini Kenya na si la kipekee, kwani ni la kawaida katika nchi nyingine zinazoendelea, na hii ni kwa sababu, ni suala ambalo halijawahi kuzungumzwa hapo awali na sasa hivi tuko katika nafasi nzuri, kwani Serikali na washirika mbalimbali wameanza kulizungumzia na sasa tunapiga hatua,” alisema.

Kamishna Msaidizi wa Polisi Wilkister Nyaiwo kwa upande wake alitoa wito kwa kila mtu, wazazi na wasio wazazi kushiriki katika kuhakikisha watoto waliopotea wanapatikana.

“Je, mtu anatangazwa kutoweka nchini Kenya kwa muda gani? Nchini Kenya, ni baada ya miaka 7 ambapo faili inaweza kufungwa na kisha mtu ndipo atatangazwa kuwa amepotea katika jamii,” Nyaiwo alibainisha. “Huu ni mtazamo wa kisekta kuwa kila mtu anabeba wajibu katika nchi yetu, wala usiseme katu kwamba, wewe si mzazi na hivyo hujali iwapo mtoto anapopotea au la. Ni jukumu letu kuwarudisha watoto wetu nyumbani na kuwaweka salama pamoja na kuwalinda.”

Hey, like this? Why not share it with a buddy?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *