mtoto.news

Kenya: Wasiwasi Juu ya Mmiminiko wa Watoto Walemavu Mijini

July 4, 2023

Wasiwasi umeibuka kuhusu mmiminiko wa watoto walemavu waliotelekezwa mjini Juja, Kiambu.

Dkt Marion Karimi ambaye anaendesha kituo cha uokoaji na ukarabati wa watoto walemavu alikashifu kuwa katika miaka ya hivi majuzi idadi ya watoto wenye matatizo ya kimwili imekuwa ikiongezeka. Karimi ambaye kwa sasa anakarabati watoto 177 walemavu waliookolewa kutoka sehemu tofauti za nchi alibainisha kuwa watoto hao huwa wanatumiwa vibaya na watu wasiojulikana ili kuomba omba mitaani.

Dkt Marion Karimi wa Faith and Hope Home for Special needs Children in Juja. Picha: JOHN KAMAU

“Kazi yetu ni kuwarekebisha wale ambao waliokolewa baada ya kutelekezwa na kisha kuwaunganisha na familia zao. Hata hivyo, tumebaini kwa wasiwasi kwamba idadi ya watoto inaongezeka kwa viwango vya kutisha. Serikali inafaa kuingilia kati,” Karimi alisema.

Alizungumza katika Kanisa la World Wide Ministries katika kata ya Theta siku ya Jumapili wakati wa sherehe yake ya shukrani baada ya kupokea shahada ya heshima kwa huduma yake ya miaka 17 kwa watoto walemavu nchini. Dkt Karimi alikemea kuwa watoto wengi wenye ulemavu wanateseka kimyakimya baada ya kutelekezwa na kufungiwa majumbani mwao akibainisha kuwa kundi lake limeanza kampeni ya kuwahamasisha wazazi wenye watoto hao kuhusu haja ya kuwafichua ili wapate usaidizi.

“Kuna msaada hapa kwa watoto walemavu na wazazi wao, kuna mashirika yasiyo ya kiserikali na serikali ambayo yako tayari kusaidia kukarabati na kusomesha watoto. Kuna fursa za kusaidia watoto kukua na hata kutimiza ndoto zao kwa sababu wao pia wana talanta,” alisema.

Aidha, Dkt Karimi alibainisha kuwa, wazazi wenye watoto hao hupitia changamoto katika kuwatunza ikiwa ni pamoja na kuwapa mahitaji yao ya kimsingi, Karimi aliitaka serikali ya kitaifa na kaunti kufikiria kuweka vituo vya kuwarekebisha walemavu katika kaunti zote ndogo ambapo wanaweza kuhudumiwa kadri iwezekanavyo.

Maoni yake yaliungwa mkono na Kasisi Francis Muhia aliyewataka wazazi kutowaficha watoto wao walemavu. Muhia pia aliiomba serikali kufanya afua zitakazowezesha kusomesha watoto wenye ulemavu akibainisha kuwa shule chache zinatoa mafunzo kwa watoto wenye ulemavu wa viungo nchini na chache zilizopo zina gharama kubwa.

Aaron Gachanja ambaye anafanya kazi katika kituo cha uokoaji alisema kwamba, ili kusaidia vilivyo na kuwawezesha walemavu, jamii lazima iwakumbatie watoto hao pamoja na familia zao na kusaidia kumaliza unyanyapaa ambao wazazi wengi wanakumbana nao. “Wanaamini kwamba, kuwa na mtoto mlemavu ni laana na ndio maana wengi wao huwatelekeza hospitalini, mitaani au hata kuwafungia majumbani mwao. Ni lazima tuwakumbatie na kuwapa usaidizi unaohitajika,” Gachanja alisema.

Hata hivyo afisa mmoja wa watoto katika kaunti ndogo ya Juja ambaye aliomba hifadhi ya jina alisema kuwa suala hilo linachunguzwa ili kubaini watu ambao wamekuwa wakiwaleta watoto hao mjini mapema asubuhi. “Waliookolewa kwa kawaida hupelekwa kwenye kituo cha uokoaji ili kupata usaidizi tunapoanzisha mahusiano na familia zao kwa ajili ya kuungana nao tena,” afisa huyo alisema. 

                                                          Nakala Kutoka Star

Hey, like this? Why not share it with a buddy?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *