mtoto.news

Isiolo: Mauaji ya watoto Wawili

June 21, 2022

Mwanamke mmoja na watoto wake wawili wenye umri wa miaka miwili, na mwengine minane wameuawa kwa kupigwa risasi na wavamizi katika kijiji cha mbali katika kaunti ndogo ya Merti, Isiolo.

Shambulizi hilo lilitendeka hapo jumamosi tarehe 18 mwezi juni, katika eneo la Dogogicha mwendo wa saa 5.30 asubuhi.

Jirani aliyetoka nje ili kutafuta punda wake walioibiwa pia aliuawa.

Kulingana na The Standard mwanamke huyo alifariki kutokana na majeraha ya risasi alipokuwa akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Merti. 

Kamishna wa Kaunti ya Isiolo Geoffrey Omading alisema kuwa, shambulio hilo lilifanyika katika kijiji cha Aliomatuma karibu na mji wa Merti.

Polisi wanawasaka washukiwa hao katika maeneo ya Wajir Magharibi, Eldas, Laisamis, Saku na North Horr.

Bw Omading alisema kwamba, takriban mifugo 1,000 waliibiwa katika uvamizi huo. 

“Uchunguzi wa awali unaonyesha nia ya wavamizi hao ilikuwa kuiba lakini cha kusikitisha ni kuwa waliwaua watoto wadogo na mama yao,” alisema. 

Bw Omading aliongezea “Tuna usalama wa kutosha Merti na kaunti jirani za Marsabit na Wajir.” Siku kumi zilizopita watu watano waliuawa katika eneo moja.

Ndani ya miaka miwili na zaidi, Takriban watu 100 na zaidi wameuawa katika maeneo ya kaunti ndogo ya Merti ya Kom, Biliqo, Bassa na Yamicha.

Viongozi wa Isiolo wamekubaliana kwa kauli moja kulaani mauaji ya hivi punde. 

Mwaniaji wa ugavana wa Jubilee Abdi Guyo, mwenzake wa ODM aliyekuwa bosi wa EACC Halake Waqo na Mwakilishi wa Kike Mumina Gollo pamoja na aliyekuwa Mbunge wa Isiolo Kaskazini Joseph Samal walitoa wito kwa Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i kushughulikia hali ya ukosefu wa usalama katika kaunti ya Isiolo

Viongozi kutoka Isiolo hapo awali walikashifu ongezeko la ukosefu wa usalama katika kaunti hiyo ambao umesababisha kupoteza maisha na mifugo.

Wanahabari Wakiutubia hapo jijini Nairobi wiki jana, walisema kwamba, kumekuwa na mashambulizi kadhaa katika mwezi uliopita. 

Walidai kuwa, mashambulizi hayo yanaonekana kuratibiwa katika kaunti jirani.

Mwandishi-Khadija Mbesa

Hey, like this? Why not share it with a buddy?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *