mtoto.news

Mswada wa Watoto 2021- Umri wa Uwajibikaji Waongezwa kutoka Miaka 8 Hadi 12

July 18, 2022

Mtoto yeyote aliye chini ya miaka 12 nchini Kenya sasa anachukuliwa kuwa hana uwezo wa kutenda kosa la jinai.

Tangu mwaka wa 2001, Kenya imepata maendeleo makubwa katika kukuza haki za watoto, ikiwa ni pamoja na kuweka sera, mifumo na miundo ya kusaidia malezi ya watoto, ulinzi na ushiriki.

Hata hivyo, bado kumekuwa na mapungufu na changamoto kwa watoto wa Kenya kutambua haki zao kikamilifu, na hivyo kuhitaji marekebisho ya sera na sheria mara kwa mara.

Muswada wa Sheria ya Mtoto (2021) unaendelea katika kuimarisha ulinzi na ukuzaji wa watoto wote kwa kuzingatia masharti ya Katiba ya 2010.

Mswada huo pia unatambua haki za kimsingi za watoto kama kundi lililo katika mazingira magumu.

Mnamo Alhamisi tarehe 7, Rais Uhuru Kenyatta ametia saini sheria inayozingatia kuongezwa umri wa uwajibikaji wa mtoto kutoka miaka minane hadi kumi na miwili, vile vile sheria hii inakuza mbinu mbadala za utatuzi wa migogoro ambayo itahusiana na mtoto, na pia itatoa vikwazo kwa adhabu juu ya mtoto.

Pia itazingatia kuundwa kwa kitengo maalum cha polisi kwa ajili ya watoto pekee.

Upande wa Watoto walio na Jinsia Tofauti, au Huntha Mswada huu uliorekebishwa unasema kwamba, kutakuwa na Utambuzi wa watoto wenye jinsia tofauti yaani watoto waliozaliwa na viungo vya jinsia ya kiume na ya kike.

Watoto pia wataweza kubadilisha vyeti vya kuzaliwa kulingana na jinsia itakayokuwa na nguvu zaidi kadri wanavyokua.

Kutakuwa na nafasi salama kwa watoto wa jinsia tofauti katika taasisi mbalimbali.

Mswada huu Mpya Unalingana na Katiba kwa kutoa wajibu sawa wa mzazi kwa wazazi wote wawili yaani baba na mama wa mtoto.

Mswada huo Unatoa jukumu kwa serikali ya kaunti kushughulikia masuala ya watoto huku ikihamisha mzigo wa malezi ya watoto kwa serikali na jamii, na hivyo kutoa mwanya wa kuanzishwa kwa taasisi za kisheria za malezi ya watoto.

Muswada huu utaimarisha zaidi utawala bora wa haki za mtoto kwani unatoa fursa mbalimbali kwa ajili ya sauti ya mtoto katika masuala yote yanayowahusu na kuhakikisha ushiriki wao na ushirikishwaji wa sauti zao katika kutunga sera.

Mswada huo ni uwekezaji kwa watoto wa Kenya na ushiriki wao kamili katika maendeleo.

Mwandishi- Khadija Mbesa

Hey, like this? Why not share it with a buddy?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *