mtoto.news

Mlipuko wa surua Nchini Zimbabwe Wawaangamiza Watoto 157

August 18, 2022

Monica Mutsvangwa, Afisa wa habari amesema kwamba, mlipuko wa surua nchini Zimbabwe umewaua watoto 157, wengi wao wakiwa hawajachanjwa kutokana na imani za kidini za familia zao.

Ugonjwa wa surua uliripotiwa kwa mara ya kwanza katika jimbo la mashariki la Manicaland mapema mwezi wa Aprili na tangu wakati huo ugonjwa huo umeenea katika maeneo yote ya nchi.

Waziri wa Habari Monica Mutsvangwa amesema kwamba, angalau kesi 2,056 zimeripotiwa na takriban vifo vyote vimekuwa vya watoto ambao hawakuchanjwa.

Baraza la Mawaziri la Zimbabwe limetumia sheria inayotumika kukabiliana na majanga ili kukabiliana na mlipuko huo, aliendelea kusema.

Serikali yasema kuwa, inaanza kampeni kubwa ya chanjo inayolenga watoto wenye umri wa kati ya miezi 6 na miaka 15 na inawashirikisha viongozi wa kimila na wa kidini kuunga mkono azma hiyo.

Zimbabwe iliendelea kuwachanja watoto dhidi ya surua hata wakati wa kilele cha janga la corona, lakini harakati hiyo imetatizwa na vikundi vya kidini vinavyohubiri dhidi ya chanjo.

Madhehebu ya Kikristo yanapinga matibabu ya kisasa na yanawaambia washiriki wao wategemee wanaojiita manabii kwa ajili ya uponyaji.

Surua ni miongoni mwa magonjwa ya kuambukiza duniani na huenea zaidi angani kwa kukohoa, kupiga chafya au kugusana kwa karibu.

Dalili ni pamoja na kikohozi, homa na upele wa ngozi, wakati hatari ya surua kali au kufa kutokana na matatizo ni kubwa miongoni mwa watoto ambao hawajachanjwa.

 Milipuko ya watu ambao hawajachanjwa na walio na utapiamlo imejulikana kuua maelfu. Wanasayansi wanakadiria kuwa zaidi ya asilimia 90 ya watu wanahitaji kupewa chanjo ili kuzuia milipuko ya surua.

Shirika la Afya Ulimwenguni mnamo Aprili lilionya juu ya ongezeko la ugonjwa wa surua katika nchi zilizo hatarini kutokana na kukatizwa kwa huduma kwa sababu ya COVID-19.

Mwezi Julai, UNICEF ilisema kwamba, takriban watoto milioni 25 duniani kote wamekosa chanjo ya mara kwa mara dhidi ya magonjwa ya kawaida ya utotoni, na kuiita “tahadhari nyekundu” kwa afya ya mtoto.

Hey, like this? Why not share it with a buddy?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *