Polisi nchini Nigeria wamemkamata mwanamke mwenye umri wa miaka 44 kwa tuhuma za wizi wa watoto 15 katika jimbo la kusini la Rivers.
Polisi wanasema kwamba, watoto hao walitekwa nyara ili kuuzwa na mwanamke huyo , ambaye alidai kuwa yeye ni mtawa anayeendesha kituo cha watoto yatima.
Watoto hao wanaripotiwa kuwa na umri wa kati ya miaka minne na 15.
Polisi walisema kuwa, wanajitahidi kuwaunganisha watoto hao na wazazi wao.
Kamishna wa Polisi wa Jimbo hilo, Friday Eboka, alisema uchunguzi umebaini kuwa baadhi yao walitekwa nyara miaka iliyopita, akiwemo mtoto wa miaka tisa ambaye alichukuliwa kutoka sokoni mwaka 2020.
Alisema kuwa,baadhi ya watoto hao wamewaeleza polisi matukio yao ya kuteswa na kudhulumiwa.
Alisema kwamba, uchunguzi zaidi kuhusu tukio hilo unaendelea ili kuwakamata watuhumiwa wengine wanaohusishwa na uhalifu huo.
Usafirishaji haramu wa watoto ni jambo linalotokea kila kona ya dunia, aidha kupitia njia ya mitandaoni au isiyo ya mitandaoni, ila uhalifu huu unawaathiri mamilioni ya watoto Nchini Nigeria.
Leave a Reply