mtoto.news

Kenya: Elimu ya mtoto ipo hatarini nyakati za ukame na mabadiliko ya hali ya hewa

November 7, 2022

Huku ukame unaendelea kuathiri kaunti tofauti tofauti nchini Kenya, watoto ndio wanaoendelea kubeba mzigo mkubwa wa athari za mabadiliko ya hali ya anga

Mamlaka ya Kenya inasema kwamba, ukame unaoendelea ambao umewasababishia mamilioni ya watu kuhitaji msaada wa chakula pia unalazimisha makumi ya maelfu ya watoto kutoka jamii za wafugaji kuacha shule. Marundo ya mizoga ya wanyama waliokatwa vipande vipande yanaweza kupatikana kila mahali kufuatia ukame mbaya ambao umesababisha takriban watu milioni 4.5 kuhitaji msaada.

Katika kijiji cha Quley, kaskazini mashariki mwa Kaunti ya Wajir nchini Kenya, Nadir Mohamed mwenye umri wa miaka 11 na ndugu zake wawili kati ya wasaba waliachishwa shule mwezi Agosti ili kuchunga mifugo ya familia yao.

Mama yao, Hindiya Abdi, amesema kwamba, familia hiyo ililazimika kuhamia kwenye malisho ya kijani kibichi la sivyo wanyama hao wangefariki kutokana na kiu na njaa.

“Ningependa sana watoto wabaki shuleni, ila tulihitaji msaada wao ili katika kuchunga mifugo,” Alisema kwa kisomali.

Katika kijiji cha Karu, Sadik Dakane mwenye umri wa miaka 17 alisafiri masaa mawili chini ya jua kali ili kuweza kufika katika mojawapo ya visima vichache akitafuta maji.

“Niliacha shule punde tu ukame ulipotokea,” alisema kwa Kisomali. “Baba yangu alihama na ng’ombe wake kwenda Somalia, huku akiniacha mimi na mama yangu.”

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) lilisema katika ripoti ya mwezi uliopita kwamba, zaidi ya wanafunzi 400,000 nchini Kenya wameathiriwa na ukame na inakadiriwa kuwa 66,000 wamekatishwa masomo.

Ila hali ya elimu ya watoto inaweza kuwa mbaya zaidi.

Vyanzo vya habari viliiambia VOA kwamba makadirio rasmi ambayo bado hayajatolewa yanaonyesha kuwa, watoto 100,000 wameacha shule katika kaunti tatu pekee kaskazini mashariki mwa Kenya ambayo ni Garissa, Mandera na Wajir.

Hashim Elmoge, mwanaharakati wa utawala bora wa eneo hilo, ana wasiwasi mkuu kuhusu athari za muda mrefu katika maisha ya baadaye ya watoto.

Ili kupunguza athari za ukame, serikali na makundi ya misaada yamekuwa yakizama zaidi kwenye visima na kuleta chakula cha dharura kwa wafugaji na mifugo yao.

Hata hivyo, Jilo Roba, mratibu wa idara ya watoto katika Kaunti ya Wajir, alisema kwamba mahitaji ni makubwa mno, na juhudi za kuongeza mahudhurio ya shule miongoni mwa jamii za wafugaji wanaohamahama zinapata pigo.

“Mafanikio ambayo yamepatikana hapo awali yanabadilishwa na ukame mkali wa sasa wa La Nina,” Roba alisema.

Viongozi na wanaharakati wana wasiwasi ikiwa mvua haitanyesha hivi karibuni, itawakusudia familia nyingi za wafugaji kuwaachisha watoto wao shule, na inaweza kuchukua miezi au hata miaka ili kuwarejesha darasani.

Hey, like this? Why not share it with a buddy?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *