mtoto.news

Zaidi ya watahiniwa 300 wajawazito kukalia mitihani ya kitaifa

November 30, 2022

Takriban wasichana 317 wajawazito wamekalia mitihani ya kitaifa ya darasa la sita, nane na kidato cha nne

Takriban wasichana 317 wajawazito ni miongoni mwa maelfu ya watahiniwa wanaofanya mtihani wa Kutathmini Elimu ya Shule ya Msingi ya Kenya (KPSEA) na Cheti cha Elimu ya Msingi ya Kenya (KCPE) katika kaunti za South Rift.

 Jumla ya watahiniwa 292 wajawazito wanatoka katika kaunti ya Baringo, Bomet na Narok, huku wasichana  25 wajawazito wanatoka katika kaunti ndogo ya Naivasha. Kati ya hao 25, saba ni watahiniwa wa KCPE huku wengine 18 wakifanya mitihani yao ya KCSE katika vituo tofauti katika eneo bunge hilo kubwa.

 

Bomet

Wasichana 102 wamerekodiwa kama watahiniwa wajawazito wakati wa mitihani hiyo katika Kaunti ya Bomet. Mkurugenzi wa Elimu wa Kaunti ya Bomet Apollo Apuko amesema kwamba,18 kati ya hao watahiniwa wanafanya mitihani ya KCPE na msichana mmoja wa darasa la sita anaandika karatasi zake za KPSEA.

Bw Apollo anasema kwamba, wasichana wengine 83 wajawazito wako tayari kukalia Cheti chao cha Elimu ya Sekondari ya Kenya (KCSE) kuanzia mwezi ujao. Akizungumza wakati wa usambazaji wa vifaa vya mitihani katika bohari Kuu ya Bomet, Apuko alisema kuwa, watahiniwa 19 walioanza mitihani yao leo wamesambazwa katika vituo mbalimbali vya Sotik, Bomet Mashariki, Bomet Central Chepalungu, na Konoin.

Mkurugenzi huyo alisema kuwa, hatua stahiki za usalama zimechukuliwa ili kuhakikisha watahiniwa hao wana uwezo wa kumaliza mitihani yao. “Tunawahudumia na iwapo mmoja wao atajifungua tutahakikisha kwamba wanafanya mitihani yao hospitalini bila tatizo lolote,” alisema.

Apuko ambaye alikuwa pamoja na Kamishna wa Kaunti ya Bomet Dkt Ahmed Omar alisema licha ya visa hivyo vya ujauzito hakuna sababu ya kutisha katika kipindi hicho. Kaunti ya Bomet ina vituo 852 vya KCPE na watahiniwa 29,391 wanaofanya mitihani na vituo 911 vya KPSEA vyenye watahiniwa 28,634 mtawalia.

 

Baringo

Katika Kaunti ya Baringo, wasichana 22 walikalia mitihani yao ya KCPE wakiwa wajawazito huku Baringo Kaskazini ikiwa na akina mama 14 wajawazito. Kaunti ndogo ya Mogotio ilikuwa na wasichana wanne wajawazito, huku kaunti ndogo za Tiaty Mashariki na Baringo Kusini ziliripoti watahiniwa wawili kila moja.

Kati ya watahiniwa 12,087 wa KCSE, wasichana 48 wajawazito watafanya mitihani mwaka huu. Kamishna wa Kaunti ya eneo hilo Abdirizak Jaldesa ambaye alisimamia usambazaji wa vifaa vya mitihani katika bohari ya Mitihani ya Kabarnet alisema kwamba, zoezi hilo lilianza vizuri bila visa vyovyote.

“Mitihani imeanza katika kaunti zote saba ndogo, tumeweka mikakati ya kutosha ya usalama katika kuhakikisha kuwa watahiniwa wanapewa wakati mzuri wanapofanya mitihani yao bila changamoto,” Jaldesa alisema.

Narok

Kaunti ya Narok iliripoti kuwa jumla ya wasichana 120 wamekalia mitihani yao wakiwa wajawazito. Kamishna wa Kaunti ya eneo hilo Isaac Masinde alisema kwamba, wasichana hao wataangaliwa kwa karibu katika kipindi chote hicho ili waweze kusaidiwa inapobidi.

Aliwataka wasichana wote wajawazito kutokwepa kufanya mtihani wa kitaifa licha ya hali zao na kuongeza kuwa hata wale ambao wangewadiwa na wakati wa kujifungua wakati wa mtihani huo basi  watafanya mitihani hiyo hospitalini. “Tunataka watahiniwa wote wachukuliwe kwa usawa ili wafanye mitihani ya kitaifa kwa raha. Hakuna mtoto anayepaswa kujihisi hafai kwa sababu ya hali yake,” alisema.


Huku hayo yakijiri, katika kaunti ya Nakuru, serikali imeahidi kuchukua hatua kali dhidi ya shule zote zitakazopatikana kuhusika na makosa ya mitihani ikiwemo ubaguzi. Hii ilikuwa baada ya wasiwasi kuibuka kuwa Victonell Academy inadaiwa kuwabagua wanafunzi kulingana na utendakazi, kwa kusajili watahiniwa waliofanya vibaya katika KCPE katika shule zingine tanzu.

Kwa mujibu wa wazazi, wanafunzi wapatao 16 walisajiliwa chini ya Shule ya Langalanga Happy Child School (13) na Flamingo Primary (3) kwa sababu hawakufanya vizuri kulingana na viwango vya Victonell. Akizungumza na The Standard Mkurugenzi Msaidizi Mwandamizi wa Elimu Frederick Osewe alisema kuwa,  inasikitisha kuwa shule za aina hiyo bado zipo.

Alisema pamoja na kwamba ilikuwa vigumu kwa Wizara kugundua na kushughulikia kero hizo, lakini wamechukua hatua kuhakikisha hali hiyo haitajirudia tena. Osewe alisema kwamba, ili kuepusha usumbufu, wanafunzi watafanya mitihani katika shule walizosajili lakini watahakikisha matokeo yanakuja kwa jina la shule yao ya awali (Victonell).

Kamishna wa Kaunti ya Nakuru Gilbert Kitiyo alisema kwamba, usalama umeimarishwa vyema. Hata hivyo alisema maafisa watakuwa waangalifu ili kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa wakati wa mitihani.

Kulingana na wizara ya elimu, wasichana 741 katika shule za msingi na upili katika kaunti za South Rift walithibitishwa kuwa wajawazito.

Kati ya hao wasichana 332 wajawazito wako shule ya msingi huku 409 wakiwa sekondari. Kati ya wajawazito 741, 140 ni watahiniwa wa KCPE na 108 wa KCSE.

Zaidi ya wanafunzi 100,000 katika eneo hilo walianza mtihani wa KCPE na KPSEA siku ya Jumatatu. Jumla ya 57,816 watafanya mitihani ya KCPE huku 59,795 watafanya KPSEA katika vituo 1,087.


Nakala kutoka The Standard

Hey, like this? Why not share it with a buddy?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *