mtoto.news

Zaidi ya Watoto Milioni 3.5 Kukosa Shule mnamo Januari 2023 Kutokana na Ukame :Save The Children.

December 6, 2022

 

Picha:Thomas Mukoya/Reuters

Zaidi ya watoto milioni 3.5 nchini Kenya wako kwenye hatari ya kukosa kuenda shule wakati zitakapofunguliwa kwa muhula wa kwanza hapo Januari mwaka ujao kwa sababu ya ukame unaoendelea, shirika la misaada ya kibinadamu la Save the Children limesema.

Utafiti wa 2021 wa Global Out of School Children Initiative ulibaini kuwa kuna zaidi ya watoto milioni mbili wenye umri wa kati ya miaka minne hadi 17 ambao wamekuwa nje ya shule tangu muhula wa tatu wa 2021.

Ripoti ya Tathmini ya Mvua za Muda Mrefu na Mamlaka ya Kitaifa ya Kudhibiti Majanga (NDMA) inakadiria kuwa watoto zaidi ya milioni 1.6 wako katika hatari kubwa ya kuacha shule wakati zinapofunguliwa kwa muhula wa kwanza mwaka ujao huku janga la njaa likizidi kuwa baya.

Mandera, Garissa, Wajir, Turkana na Marsabit ni miongoni mwa kaunti zilizoathiriwa zaidi huku Mandera ikiwa na idadi kubwa zaidi ya watoto walioacha shule kati ya watoto 295,470 wenye umri wa kati ya miaka 4 hadi 17.

Garissa inashika nafasi ya pili kwa 289,410, Wajir 266,540, Turkana 253,640 kisha Marsabit 107,600 walioacha shule.

Kaunti zingine pia zilizoathiriwa pakubwa ni Narok iliyo na 83,020, Pokot Magharibi 80,070 na Samburu iliyo na wanafunzi 64,818 walioacha shule.

Ripoti ya Tathmini ya Mvua za Muda Mrefu 2022, kipindi cha makadirio ya Oktoba hadi Desemba katika eneo la Ardhi Kame na Nusu Kame (ASAL) inaonyesha kuwa watu milioni 4.35 nchini Kenya wanakabiliwa na viwango vya juu vya uhaba wa chakula.

Kulingana na utafiti wa hivi majuzi uliofanywa na shirika la Save the Children mnamo Juni 2022 kuhusu athari za ukame katika kaunti 17, kupungua kwa idadi ya wanaoandikishwa kunaonekana katika kaunti zote huku kukiwa na wastani wa asilimia 52 ya shule zilizoathiriwa katika ngazi zote Elimu ya Awali, Msingi na Sekondari).

Miongoni mwa sababu kuu za kuacha shule ya upili ziliangaziwa  ni uhaba au ukosefu wa mlo shuleni, mazingira duni ya kujifunzia, ukosefu wa walimu, uchakavu wa miundombinu, migogoro ya rasilimali na dharura zinazohusiana na hali ya hewa.

Uhaba wa maji shuleni pia ni sababu kuu. Uchambuzi wa maji katika shule za msingi na upili katika kaunti 17 zinazolengwa na sekta ya elimu umebaini kuwa shule 460 hazina vyanzo vya maji na shule 1,896 zinategemea tu kuvuna maji ya mvua.

“Kenya inakumbwa na ukame mbaya zaidi kuwahi kutokea katika kipindi cha miaka 40. Watoto ndio vikundi vilivyo hatarini zaidi na kwa kawaida ndio huathirika zaidi katika dharura kama hizo. Wazazi wanapaswa kuhama na watoto wao kutafuta chakula, malisho na maji ya mifugo yao. Hii inahatarisha upatikanaji wao wa vifaa vya msingi kama vile chakula, maji safi, huduma za afya na elimu,” alisema Yvonne Arunga, Mkurugenzi wa Nchi wa Shirika la Save the Children Kenya na Madagascar.

Kaskazini mwa Kenya, wazazi wengi hawawezi kulipa karo kwa sababu wamepoteza vyanzo vyao vya kujikimu kutokana na ukame.

Jamii zimezingatia zaidi ujuzi wa kimsingi wa kuishi na watoto wanaoenda shule wanapaswa kuwasaidia wazazi wao kutunza mifugo na kufanya kazi za nyumbani.

Shirika la Save the Children pia limeiomba serikali kuhakikisha kunakuwa na huduma ya maji safi na salama ya kunywa, usafi wa mazingira na usafi wa kibinafsi shuleni pamoja na mlo wa bure shuleni wakati wa ukame kwa madhumuni ya kuimarisha mazingira bora ya shule yatakayowafanya watoto kuendelea na masomo.

Aidha Shirika hilo liliitaka serikali kuweka mifumo ya ufuatiliaji wa wakati halisi ili kutathmini hali shuleni mwanzoni mwa ukame ili kuwezesha majibu ya mapema kabla ya athari za kufungwa kwa shule kujitokeza.

Ili kukabiliana na mapungufu haya katika elimu, Shirika la Save the Children linatekeleza Mradi wa Operesheni wa kwenda Shuleni uliopewa jina ‘Watoto Rudi Shule’ ili kuongeza uandikishaji na uhifadhi wa watoto ambao hawajaenda shule katika Kaunti za Wajir Turkana, Baringo na Bungoma.

Shirika hilo litafanya kazi kwa ushirikiano na idara mbalimbali ikiwemo Wizara ya Elimu, Tume ya Huduma ya Walimu, Idara ya Vijana, Jinsia na Huduma za Jamii, Kurugenzi ya Elimu ya Kaunti, na Afya ya Umma pamoja na washikadau wengine wa elimu katika Kaunti zinazolengwa. Hii itahakikisha ulinganifu na vipaumbele vya ngazi ya kaunti na vipaumbele vya elimu ya mradi katika mradi uliopendekezwa.

Shirika la Save the Children linatoa usaidizi wa kuokoa maisha kwa watoto na familia zao zilizoathiriwa na ukame katika Kaunti za Turkana, Mandera, Wajir na Garissa kupitia afya, lishe, usalama wa chakula, ulinzi wa watoto, usafi wa maji, usafi wa mazingira na afua za elimu.

Shirika hilo limefikia watu 737,931 wakiwemo watoto 405,511 mwaka huu.

Hey, like this? Why not share it with a buddy?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *