mtoto.news

Sababu Kuu Zinazoleta Mfadhaiko na Dhiki kwa Watoto

January 25, 2023

Je, Wewe kama mzazi utafanya nini iwapo utaona dalili za mafadhaiko kwa mtoto wako???

Watu wazima wengi hua na mafikira ya kwamba, utoto na ujana ndio wakati ulio na furaha zaidi maishani, ila ukweli ni kwamba, watoto wengi na vijana wana uwezekano mkubwa wa kupata mateso ya dhiki na mafadhaiko ambazo huweza kusababisha unyogovu kwa watoto hao.

Uchunguzi unaonyesha kuwa, kwa kila vijana wanne, kuna uwezekano wa kijana mmoja kati yao kupatwa na mfadhaiko kabla ya kufikisha umri wa miaka 19, sababu zake zikishinikizwa na marafiki, dhiki na wasiwasi shuleni na mengine mengi.

Sababu za kawaida za dhiki kwa vijana

1. Shule

Watoto wengi huwa na hamu ya kuweza kufanya vyema shuleni, huku wazazi pia wakiwashinikiza watoto wao wapate alama nzuri shuleni. Isitoshe, watoto wengi hulemewa na kazi za shuleni ikiongezwa na kazi za nyumbani. Zaidi ya hayo, iwapo mtoto atafeli ama atakaposhindwa kumaliza kazi zake kwa wakati, basi hujawa na dhiki na mfadhaiko, vile vile, mara nyingi watoto hawa hukosa hata muda wa kwenda kucheza, hii ikifanya hisia zao ziwe chini mno.

2. Mitihani

Mitihani inaweza kuwaweka watoto na vijana chini ya shinikizo, na kulingana na Childline, watoto walio na umri wa miaka 12-15 wana uwezekano mkubwa wa kuomba msaada kuhusu mafadhaiko ya mitihani. Baadhi ya sababu kuu ni kwamba, watoto wengi wanaogopa kufeli mitihani kwani hawapendi  kuwakatisha tamaa wazazi wao, na kwa sababu hiyo, wale waliowasiliana na Childline walisema kwamba mkazo wao wa mtihani ulikuwa unasababisha mfadhaiko, wasiwasi, mashambulizi ya hofu na kutojistahi.

3. Shinikizo la rika  

(peer pressure)

Watoto wengi hupata shida katika kutengeza au kupata marafiki, na wengi wao huhisi upweke mno huku wakijilazimisha kuwa na tabia na mienendo sawa na watoto wengine ndiposa waweze kupata marafiki. Jambo ambalo huwafanya watoto watende mambo ambayo hayatawapatia furaha yoyote ile.

4. Uonevu na Unyanyasaji

Kulingana na shirika la misaada la Young Minds , uonevu na unyanyasaji huathiri zaidi ya vijana milioni moja kila mwaka. Kama mzazi, kuna mambo fulani unayoweza kuangalia ambayo yanaweza kuonyesha kwamba mtoto wako ananyanyaswa na kuonewa.

Haya ni pamoja na kujitenga na woga, kutofaulu shuleni, kujifanya mgonjwa ili asiende shule, kutokula au kulala vizuri na kuwa na majeraha yasiyoelezeka kama vile michubuko.

5. Matukio ya ulimwengu

Ni vigumu mno kuwaficha watoto kutokana na habari mbaya kama vile vita, majanga na ukatili wa kila aina siku hizi. Na hivyo, baadhi ya watoto wanaweza kuwa na wasiwasi kuhusu usalama wao na wa wazazi wao, wanafamilia na marafiki.

6. Shida za familia au mabadiliko kwenye familia

Kuhamia maeneo mapya au nyumba mpya, au wazazi kutengana, matatizo ya kifamilia na mabadiliko kadha wa kadha yanaweza kuwa magumu kwa mtoto au kijana na inaweza kusababisha dalili za dhiki.

Vidokezo vya kumsaidia mtoto wako katika kukabiliana na mafadhaiko na wasiwasi

Tenga wakati wako kwa ajili yao

Wazazi wote wana shughuli nyingi siku hizi, lakini ni muhimu kutenga muda wako ili uwe na ukaribu na mtoto wako, hasa unapoona dalili za wasiwasi, dhiki na mfadhaiko kwa mtoto wako. Waulize watoto wako kuhusu siku yao na uonyeshe kupendezwa na mambo ambayo ni muhimu kwao. Lakini jaribu kuzuia kuwalazimisha kuzungumza kuhusu dhiki na wasiwasi wao, kuwa na imani na wao na kwa hakika  watafunguka wakati wanahisi ni salama kwao kuzungumza juu ya shida wanazozikumba.

Kuhimiza usingizi wenye afya

Iwapo watoto wataweza kupata muda muafaka wa kulala na kupumzika inavyofaa, basi watoto hao wanaweza kustahimilia mafadhaiko. Watoto wanahitaji muda tofauti wa kulala katika umri tofauti.

Wape chakula cha afya

Jaribu kuhakikisha kuwa watoto wanakula angalau sehemu tano za aina mbalimbali za matunda na mboga kila siku. Ikiwa watoto wako ni sugu kwa kula matunda na mboga, kuna njia nyingi za uvumbuzi za kuwaingiza kwenye lishe bora.

Mafunzo ya kuonyesha kuwa Mafadhaiko ni jambo la kawaida

Inaweza kuwa na manufaa kuwakumbusha watoto wako kwamba kiwango fulani cha mfadhaiko ni cha kawaida kabisa maishani, na kwamba kila mtu anaathiriwa nacho na inabidi atafute njia za kukabiliana nacho. Waelezee kuwa ni sawa kuhisi kile wanachohisi maana hiyo inaweza kuwapa ujasiri wanaohitaji katika kudhibiti viwango vyao vya mafadhaiko. Aidha, jaribu kuzungumzia nyakati ambazo umekuwa na dhiki na mfadhaiko, na ueleze jinsi ulivyokabiliana na hali hiyo.

Wachangamshe 

Mazoezi ya kimwili yanaweza kusaidia watoto na watu wazima katika kudhibiti mfadhaiko, kwa hivyo hakikisha watoto wako wanafanya mazoezi mengi. Mambo mengine unayoweza kujaribu ni pamoja na mbinu za kupumzika na hata vitu kama mazoezi ya kupumua.

Hata hivyo, la muhimu kabisa ni uelewa wako na uwepo wako wakati mtoto wako anaonyesha dalili za mfadhaiko na dhiki.

Hey, like this? Why not share it with a buddy?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *