mtoto.news

Mitindo Minane Itakayoathiri Watoto Mwaka wa 2023

January 31, 2023

UNICEF/UN118890/QUARMYNE

Msururu wa migogoro iliyounganishwa inatarajiwa kuwa na athari kubwa kwa watoto mwaka wa 2023. Ripoti kutoka shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF), iliyotolewa Jumanne, inaeleza kwa kina mielekeo ambayo itabadilisha maisha yao katika kipindi cha miezi 12 ijayo.

Ripoti hiyo, “Matarajio ya Watoto Mwaka 2023: Mtazamo wa Ulimwenguni”, pia inaangalia anuwai ya maeneo mengine muhimu, kutoka kwa athari inayoendelea ya janga la COVID-19 hadi kugawanyika kwa mtandao, na dharura ya hali ya hewa. 

Haya ndiyo maarifa manane yaliyomo ndani ya utafiti huo.

1) Athari za Covid -19 Zimekuwa mbaya mno ila mafanikio ya kiafya yanatoa tumaini

Janga la COVID-19 limeangazia hitaji la usalama thabiti wa afya ulimwenguni na nchi nyingi bado ziko hatarini. Kwa bahati mbaya, mara nyingi ni watoto ambao huwa hatarini zaidi, ikiwa sio kwa virusi vyenyewe, basi ni kwa athari zake nyingi.

Wakati huo huo, janga hili limechochea maendeleo ya kushangaza katika ukuzaji wa chanjo na mageuzi katika mifumo ya afya ya kimataifa na, mnamo 2023, ni muhimu ulimwengu uendelee kuimarisha usanifu wa afya kote ulimwenguni.

 

2) Juhudi za kudhibiti mfumuko wa bei zina athari zisizotarajiwa kwa umaskini wa watoto

Kupanda kwa mfumuko wa bei imekuwa hadithi ya kiuchumi ya mwaka huu na bila ya kushangaza, athari zake zinaweza kulemea familia na watoto. Majaribio ya kudhibiti kupanda kwa bei pia yanaweza kuwa na matokeo mabaya, kama vile kupunguza ukuaji wa uchumi na kupunguza nafasi za kazi hasa kwa vijana.

Hatua ya serikali ya kupanua na kulinda manufaa ya kijamii, huwaepusha walio hatarini zaidi kutokana na athari za kubana uchumi. 

3) Ukosefu wa usalama wa chakula na lishe unaonekana kuendelea

Ukosefu wa usalama wa chakula umekuwa ukiongezeka kutokana na matukio mabaya ya hali ya hewa, vikwazo katika minyororo muhimu ya ugavi, na migogoro kama vile vita nchini Ukraine. Kadiri bei zinavyopanda, familia nyingi zaidi ulimwenguni hupata ugumu wa kulisha watoto wao, hali iliyo na uwezekano wa kuendelea mwaka 2023.

Kufanya mifumo ya chakula duniani kuwa thabiti zaidi, ni njia mojawapo ya kupunguza suala hili.

4) Migogoro ya nishati husababisha madhara ya haraka, lakini kuzingatia uendelevu kunamaanisha kwamba, siku zijazo zitakuwa na nuru.

Kwa mabilioni ya watu, kupanda kwa bei ya nishati kunaongeza sana gharama ya maisha, na mtazamo wa 2023 hauna uhakika katu. Mtazamo huo umechochea umakini mkubwa zaidi katika mpito hadi vyanzo vya nishati safi na endelevu, na uwezekano wa kuunda ajira mpya kwa vijana.

Hata hivyo, wengi wao hawako tayari kwa kazi hizi mpya, kwa hivyo, suala la kuwatayarisha vijana wanaotafuta kazi na fursa za mafunzo, lahitaji kuwa sehemu muhimu ya ajenda yoyote ya nishati ya kijani.

5) Kuzingatia fedha za hali ya hewa na katika kusaidia nchi zinazoendelea kupata nafuu ya madeni

Nchi zinazoendelea zinakabiliwa na changamoto nyingi zinapojaribu kupata nafuu kutokana na janga hili, kushughulikia mzozo wa hali ya hewa na kukabiliana na matatizo ya kiuchumi, lakini msaada wa kifedha kwa nchi hizi hauongezeki ilhali mahitaji yao yanaongezeka.

Bila mageuzi ya kufungua fedha za ziada za maendeleo, rasilimali zitaenea zaidi na mahitaji ya dharura yataachwa bila kutimizwa na hiyo ni habari mbaya kwa watoto.

6)Demokrasia iko chini ya tishio na harakati za kijamii zinarudi nyuma

Demokrasia imezidi kuhatarishwa katika miaka ya hivi karibuni, na itaendelea kupingwa mwaka 2023. Kukosekana kwa utulivu wa kisiasa kunaweza kusababisha mabadiliko chanya ya kijamii, lakini pia kunaweza kuacha milango wazi kwa viongozi wa kimabavu.

Mnamo 2023, kuna uwezekano kwamba vijana watakuwa na jukumu kubwa zaidi katika harakati za kijamii, iwe katika hali ya hewa, afya ya akili, elimu, au usawa wa kijinsia. Utetezi wao utakuwa na nguvu na utachangia kasi ya mabadiliko.

7) Kuongezeka kwa uadui kunatatiza juhudi za kuwasaidia watoto

Katika mazingira ya kuongezeka kwa ubinafsi wa kikundi, ushirikiano wa pande nyingi unakuwa mgumu zaidi, huku idadi ya watoto wanaohitaji msaada kwa sasa iko katika kiwango cha juu tangu Vita vya Pili vya Dunia, na ulimwengu ulio na upinzani mara kwa mara, hauwezi kuwa na matokeo mazuri kwa watoto.

Ushirikiano ulioboreshwa wa kimataifa unahitajika ili mashirika ya kimataifa yaweze kukabiliana na changamoto zinazowakabili watoto, bado kuna fursa za kuweka mivutano kando, kutafuta maelewano na kuweka kipaumbele kwa ustawi wa watoto.

8) Mtiririko wa bure wa habari mtandaoni sasa uko chini ya tishio, hii itaweza kusababisha tofauti zaidi kwa watoto

Mambo ya kiteknolojia, kibiashara na kisiasa, yanagawanya wavuti katika visiwa vilivyotengwa vya muunganisho na utawala.

Watoto huathirika zaidi kwa vile wanategemea sana mtandao kwa elimu na mwingiliano wa kijamii. Mnamo 2023, tunaweza kuona juhudi za kutangaza wavuti isiyolipishwa, jumuishi na salama, na fursa zote za kuunda mustakabali wa kidijitali unaonufaisha watoto lazima zitumike.

Hey, like this? Why not share it with a buddy?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *