mtoto.news

Afghanistan: Takriban Watoto Milioni Moja Wanakabiliwa na Utapiamlo Mkali

May 17, 2023

Afghanistan inasalia kuwa miongoni mwa maeneo ambayo yamepata majanga mabaya zaidi ya kibinadamu duniani

Afghanistan inasalia kuwa miongoni mwa maeneo ambayo yamepata majanga mabaya zaidi ya kibinadamu duniani huku Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch katika ripoti ya hivi majuzi lilisema kwamba thuluthi mbili ya wakazi wa nchi ya Afghanistan wana uhaba wa chakula.

“Afghanistan kwa kiasi kikubwa imetoweka kutoka kwa vyombo vya habari, lakini imesalia kuwa moja ya majanga mabaya zaidi ya kibinadamu duniani,” ilisema ripoti ya HRW.

Kulingana na ripoti hiyo, baada ya kupigwa marufuku kwa wanawake wanaofanya kazi katika NGOs, mgogoro umekuwa mkubwa zaidi, huku watoto 875,000 wanakabiliwa na utapiamlo mkali. “Theluthi mbili ya wakazi wa nchi hiyo wana uhaba wa chakula, ikiwa ni pamoja na watoto 875,000 wanaokabiliwa na utapiamlo mkali. Wanawake na wasichana wanasalia kuwa katika hatari zaidi,” ilisema Human Rights Watch.

Kulingana na ripoti ya Haki za Kibinadamu, upotevu mkubwa wa misaada utawaacha Waafghanistan wengi kuwa maskini na kuwa na njaa mno. Melanie Galvin, mkuu wa lishe katika Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF), katika ujumbe wa video kwenye Twitter, alisema kuwa maelfu ya watoto walio katika mazingira magumu wanaweza kufa kutokana na utapiamlo mkali nchini Afghanistan mwaka huu pekee.

Galvin aliongeza kunena kuwa, shirika la chakula duniani linakabiliwa na pengo la dharura la ufadhili la dola milioni 21, ili kununua vifaa muhimu kwa ajili ya kutibu utapiamlo na kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wa afya kote nchini. Shirika la UNICEF pia linakabiliwa na uhaba wa chakula cha tiba kilicho tayari kutumika (RUTF), alisema.

Kulingana na Khaama Press, RUTF inachukuliwa kuwa kirutubisho muhimu cha chakula kilichotengenezwa tayari ambacho kinaweza kutibu watoto wanaosumbuliwa na utapiamlo. Miaka ya mizozo, umaskini, na uchumi uliovunjika na unaotegemea ufadhili umewalazimu watu wa kawaida kuteseka na njaa kali na uhaba wa chakula.

UNICEF katika ripoti yake ilionyesha kuwa Afghanistan ni nyumbani kwa moja ya majanga mabaya zaidi ya kibinadamu duniani. Zaidi ya watu milioni 28, wakiwemo watoto zaidi ya milioni 15, wanahitaji msaada wa kibinadamu na ulinzi mwaka huu, hii inaonyesha ongezeko kubwa la watu milioni 4 zaidi ya mwaka wa 2022.

Tangu kurejea kwa Taliban madarakani nchini Afghanistan mwaka 2021, uchumi umeshindwa kuimarika, hii ikiwaweka mamilioni ya watu kwenye hatihati ya njaa.

 

Hey, like this? Why not share it with a buddy?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *