mtoto.news

Unicef ​​yazindua programu ya kufuatilia kipindi cha hedhi kwa wasichana nchini Kenya

May 31, 2023

 

Ili kufikia wasichana wengi zaidi, programu itafanya kazi yake bila ya kuhitaji vifurushi vya data

Hedhi ni mchakato wa kawaida katika maisha ya kila mwanamke, lakini mara nyingi hufunikwa na usiri na aibu. Takriban wanawake na wasichana milioni 9.3 nchini Kenya hupata hedhi. Mara nyingi wasichana waliofikisha umri wa kubalighi hutafuta majibu kuhusu afya yao ya hedhi ila mara nyingi huambulia patupu.

Ili kukabiliana na changamoto hii, Unicef ​​imezindua ‘Oky Kenya’, toleo lililorekebishwa la programu ya kufuatilia siku za hedhi, hasa kwa kwa wasichana wanaoishi ndani ya nchi zilizo na kipato cha chini na cha kati kama vile Kenya. Unicef ​​iliunga mkono urekebishaji wa Oky ili kutoa maelezo kuhusu hedhi kulingana na mazingira ya Kenya, kwa ushirikiano na LVCT Health, Wizara ya Afya na Wizara ya Elimu.

“Mojawapo ya sababu kuu za wasichana kutafuta habari kuhusu hedhi ni kufuta hadithi na imani potofu ambazo mara nyingi husababisha wasiwasi, hofu na aibu,” Mwakilishi wa Unicef ​​nchini Kenya Shaheen Nilofer alisema. “Ningependa kuipongeza Oky Kenya kwa kutengeneza programu bunifu kwa wasichana wa Kenya. Hii itasaidia kuvunja vikwazo na kuwawezesha wasichana kuchukua udhibiti wa afya zao na maisha yao.”

Kutoa taarifa kuhusu hedhi ni muhimu kwa ajili ya kukuza usawa wa kijinsia na kuwasaidia wasichana kuridhika na mabadiliko wanayopitia huku wakiendelea kuishi maisha marefu.

Katika maeneo mengi ya vijijini na makazi yasiyo rasmi, hasa pale ambapo kuna uhaba wa maji safi na usafi wa mazingira, hedhi inaweza kuwa kikwazo kwa elimu ya wasichana, kwani mara nyingi wasichana hukosa shule kwa sababu ya kukosa huduma za usafi au kuogopa aibu.

Oky Kenya itawapa wasichana taarifa zinazofaa na zenye msingi wa ushahidi kuhusu vipindi vyao vya hedhi kwa njia za kufurahisha, bunifu na chanya, kupitia simu za mkononi. Ili kufikia wasichana wengi zaidi, programu itafanya kazi yake bila ya kuhitaji vifurushi vya data.

Programu hiyo inapatikana kwa simu za Android, kutoka Google Play, na inapatika kwa Kiingereza na Kiswahili nchini Kenya. Hata hivyo, programu hiyo inatazamiwa kupatikana hivi karibuni katika umbizo la iPhone na kompyuta kibao.

Hey, like this? Why not share it with a buddy?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *