mtoto.news

Uzinduzi wa Mpango Wa Kuwalinda Watoto Dhidi Ya Ukatili

June 21, 2023

Maandamano kwenye barabara kuu ya Kakamega Webuye wakati wa Uzinduzi wa programu ya Tetea. Picha:CISP twitter

 

Kamati ya Kimataifa ya Maendeleo ya Watu (CISP) imezindua mradi wa Tetea hapo jana tarehe 20 mwezi juni, unaofadhiliwa na Muungano wa Ulaya wa kulinda wanawake na watoto dhidi ya dhuluma katika Kaunti ya Kakamega.

Mradi huo utatekelezwa na CISP kwa ushirikiano na Shirika Lisilo la Kiserikali la eneo hilo, Kakamega County Widows Empowerment Project (KCWEP) na Men Engage Kenya Network (MENKEN). Mradi huo wa miaka mitatu unalenga kupunguza visa vya mimba za utotoni na kuwalinda watoto na wanawake dhidi ya Unyanyasaji wa Kijinsia  (SGBV) katika Kaunti Ndogo za Shinyalu na Malava kaunti ya Kakamega.

Afisa wa programu wa CISP Bi Esther Waduu alisema kwamba, tathmini ya haraka iliyofanywa na shirika hilo pamoja na data iliyopatikana kutoka kwa idara ya huduma kwa watoto ilionyesha kuwa kaunti ndogo za Malava na Shinyalu zinaongoza kwa visa vya unyanyasaji wa watoto, SGBV, mimba za utotoni na ndoa za mapema.

Mradi huo utatekelezwa kupitia midahalo ya Kijamii na jamii zinazopata mafunzo kwa muda wa wiki 13 na baada ya hapo watatoa tamko la umma kuhusu jinsi watakavyolinda watoto na wanawake. Washirika pia wataanzisha vilabu vya kutetea haki za Mtoto shuleni kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu ili kuwawezesha watoto kuelewa haki zao za kuripoti au kutafuta msaada kwa urahisi wanapodhulumiwa.

Hatutawaacha walionusurika nyuma, kwa sababu wapo ambao tayari wana watoto na wengine wenye mimba na kwa ajili yao, tutaanzisha vikundi ili kuhakikisha wanasaidiwa na pia kupata vifaa vya utu ili tuwafanyie bidii ndipo warudi shule na wengine wapelekwe shule za ufundi ili kujikimu wao na watoto wao – Bi Esther Waduu

Katika kuimarisha mifumo ya walionusurika kupata huduma bora, washirika katika mradi huo utawapa mafunzo washikadau na kuwaratibu ili kuhakikisha kesi zinaendeshwa kwa ufanisi. KCWEP, ambayo inafanya kazi na wajane, itashiriki katika kuleta kaya zinazoongozwa na wanawake katika mikoa inayolengwa ya utekelezaji wa mradi ili kusimama kidete na kutunza familia zao.

Hata hivyo, mkurugenzi wa KCWEP Mwanzi Jerry alisema kuwa,  kaya zinazoongozwa na wanawake hulengwa kirahisi na wahalifu wa kijinsia.

Tunawataka waelewe kwamba kama kaya zinazoongozwa na wanawake, watoto wao pia hupitia unyanyasaji kwa sababu familia ikiwa katika mazingira magumu ambayo hukosa kuwapatia mahitaji yao ya kimsingi basi utaona wanaume ndio wahusika wa kipaumbele cha kwanza kuwadhulumu watoto hao. . Kwa hivyo tunawahamasisha wanawake kuchukua nafasi zao kama wanawake wakuu wa kaya ili kuhakikisha wanapunguza visa vya ukatili wa kijinsia – Mwanzi Jerry.

Wanaume pia watahusishwa wakati wa mradi wa kuwa mabingwa wa kutetea haki za wanawake na watoto na pia kuwalinda dhidi ya aina yoyote ya unyanyasaji. Kulingana na Amos Simpano kutoka Mtandao wa Men Engage Kenya (MENKEN), shirika litaangalia sera na kuzirekebisha ili kuwajengea uwezo wanaume kupambana na visa vya unyanyasaji wa kijinsia.

“Tunaamini kuwa, kama wanaume, sisi ni viongozi katika familia na utamaduni unatupa nafasi ya juu zaidi na tunaamini kwamba wanaume wanapoamua kutetea haki za wanawake na watoto, basi itakuwa rahisi kushughulikia tatizo hilo,” alibainisha.

Hey, like this? Why not share it with a buddy?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *