Watoto watatu ni miongoni mwa watu wanane waliouawa katika kijiji cha Yell Kurkum huko Laisamis, Kaunti ya Marsabit.
Kulingana na polisi, washambuliaji walifyatua risasi na kuwaua wanane hao ambao kati yao kulikuwa na wanaume watano, pamoja na watoto watatu.
Kamanda wa polisi wa Mashariki Rono Bunei anasema kuwa, takriban majambazi 15 waliokuwa na bunduki walivamia kijiji hicho mwendo wa saa kumi na mbili asubuhi hapo jana tarehe 12. Aliongeza kunena kwamba, uvamizi huo ulianza usiku na kuendelea hadi saa za asubuhi.
Aliongezea akisema kuwa, watoto hao walikuwa na umri wa chini ya miaka 10. “Miili iligunduliwa baadaye Alhamisi baada ya shambulio, na wavamizi hao waliweza kutoroka pamoja na mifugo wengi mno na juhudi za kuwatafuta bado zinaendelea,” alisema.
Aidha, wawili kati ya waliojeruhiwa walipelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Marsabit huku mmoja wa waathiriwa akitarajiwa kusafirishwa kwa ndege hadi Nairobi kwa matibabu maalum. Timu ya mashirika mengi ya usalama ilitumwa kuwafuata washambuliaji huku maafisa zaidi walipangwa kuzuru eneo hilo Ijumaa kama sehemu ya juhudi za kushughulikia mzozo huo.
Hii si mara ya kwanza katika kutokea kwa mashambulizi haya katika kaunti ya marsabit, na pia kuna uwezekano mkubwa kuwa, jambo hili halitakua la mwisho iwapo serikali haitachukua hatua ya kuwalinda wananchi kutokana na vurugu, mashambulizi na migogoro ya aina yoyote ile.
Marsabit ni moja wapo ya maeneo yaliyo chini ya tishio kuu kutoka kwa majambazi. Mashambulizi kama haya ni ya kawaida kwani wavamizi huleta vurugu kwa sababu ya mifugo na mwishowe husababisha vifo na majeruhi, na kuna hofu kwamba ukoo ulioathiriwa utalipiza kisasi.
Hali ya wasiwasi imesalia katika eneo hilo huku maafisa wa usalama wakikimbilia huko kudhibiti mashambulizi zaidi.
Leave a Reply