mtoto.news

Uganda: Yoweri Museveni Alaani shambulizi, Anatoa Pole kwa Familia za Wanafunzi Waliopoteza Maisha

June 19, 2023

Familia katika mji wa mpakani nchini Uganda zimeanza kuwazika wapendwa wao waliofariki kwenye shambulizi hilo.

Kila mtoto ana haki ya kuishi na serikali lazima ihakikishe kwa kadiri iwezekanavyo maisha mema na ukuaji wa mtoto, lakini hilo linatiliwa shaka wakati mashambulizi ya waasi wa ADF yalipogharimu maisha ya watoto 42 wasio na hatia usiku wa Juni 16, 2023.

Kwa mujibu wa polisi, shule ya sekondari ya Lhubirira iliyoko Mpondwe iliyoko kilomita 2  kutoka mpaka wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ilivamiwa na wanachama wa Allied Democratic Forces (ADF) — kundi la Uganda lililoko mashariki mwa Kongo.

Gazeti la Daily Monitor lilimnukuu afisa mkuu wa kijeshi akisema kuwa wavulana waliofariki walikuwa wamefungiwa katika bweni moja, ambalo lilichomwa moto, huku wasichana nao wakikatwakatwa kwa mapanga katika bweni jingine. Baadhi ya wahasiriwa waliuawa kwa kupigwa risasi, na wanafunzi 6 walitekwa nyara.

Rais wa Uganda, Yoweri Museveni amelaani shambulizi hilo la Ijumaa huku akitoa pole kwa familia za wanafunzi waliopoteza maisha, na kulihakikishia taifa kuwa utambulisho wa genge hilo la uhalifu utafichuliwa.

“Ukatili huu mpya wa wanachama wa ADF ni wa uhalifu, wa kukata tamaa, wa kigaidi na ubatili. Tangu Operesheni Shujja ianze, Jeshi la Kongo na Jeshi letu limeweka shinikizo kubwa kwa ADF ambao walikuwa wamegeuza eneo hilo kuwa eneo lao kwa karibu miaka 20,” Museveni alisema.

Alisema kwamba, kundi hilo linaaminika kuweka kambi upande wa Magharibi na Kusini mwa Mlima Ruwenzori na kusababisha maafa kwa jamii inayozunguka eneo hilo.

Hata hivyo, Rais Museveni alisema kwamba, serikali ishafanikiwa kuwamaliza wahalifu 26 na kuwakamata 25, isitoshe serikali imeweza kunasa bunduki 2 nyepesi na 7 za IED.

Aidha, familia katika mji wa mpakani nchini Uganda zimeanza kuwazika wapendwa wao waliofariki kwenye shambulizi hilo.

Hey, like this? Why not share it with a buddy?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *