Je unaweza vipi kumlinda mtoto wako asilawitiwe? Au utangoja uje kujenga ukuta badala ya kuziba ufa?
Mara nyingi wazazi katika jamii zetu husahau kwamba, watoto ndio walio hatarini zaidi ya kulawitiwa, ila wengi wao hutia pamba masikioni wakajifanya hamnazo hadi wakati watoto wao watakuwa waathiriwa wa udhalilishaji wa kijinsi au kingono.
Bila shaka, Kinga ni bora kuliko tiba, ni muhimu kutambua kwamba mara nyingi wanyanyasaji huwa na tabia ya kutumia mchakato wa hila unaoitwa “grooming” ili kupata uaminifu wa familia. Ukimkosesha upendo mtoto wako, basi mnyanyasaji atanyakua nafasi hiyo kwa kumpa mtoto huyo mambo anayokosa nyumbani, kwa kujaza mahitaji na majukumu ya mzazi.
Kwa hakika hili ni jambo moja tu kati ya mengi yanayochochea udhalilishaji wa watoto kingono au kijinsia. Lakini Jukumu lako kama mzazi ni kuhakikisha kwamba, unampa mtoto wako upendo na umakini. Je unamjulia hali mtoto wako mara kwa mara, je ukona ukaribu naye na ukona upendo naye? Mtoto wako akiwa na suala lolote linalomsumbua, je anakuja kwako kukuelezea??…Kinga bora zaidi ni kuwa na uhusiano wa karibu na upendo na mtoto wako.
Jambo la pili muhimu ni kutambua kwamba, kuna uwezekano mkubwa zaidi kwamba mnyanyasaji wa mtoto wako ni mtu wa familia au mtu aliye karibu nawe.
Simulizi ya kawaida ni kwamba unyanyasaji wa kijinsia wa watoto hufanywa na watu wasiowajua. Lakini ukweli ni kwamba, watoto wengi hunyanyaswa na marafiki zetu, wapenzi wetu, wanafamilia na hata jamii. Takriban asilimia 93 ya watoto ambao ni waathiriwa wa unyanyasaji wa kijinsia wanajua wanyanyasaji wao, huku zaidi ya asilimia 10 ya watoto wanaonyanyaswa kingono wananyanyaswa na mtu wasiyemjua.
Data yasema kwamba, asilimia 50 ya watoto waliothiriwa wakiwa chini ya miaka sita waliathiriwa na wanafamilia. Vile vile, wanafamilia pia walichangia asilimia 23 ya wale wanaowanyanyasa watoto wenye umri wa miaka 12 hadi 17.
Weka mipaka sahihi kati ya mtoto wako na wanafamilia, wapenzi na hata jamii na iwapo tokeo la unyanyasaji wa mtoto wako na mtu wa karibu kwako litatokea, basi usikae kimya! Ongea.
Wazazi wengi wanapenda kusema maneno haya…Asiyefunzwa na mamaye, hufunzwa na ulimwengu..lakini ni ulimwengu upi utamfunza mtoto wako? Ni ulimwengu upi utamlea mtoto wako? Ulimwengu umejaa udhalilishaji..Chukua jukumu lako na umlinde mtoto wako dhidi ya wanyanyasaji, wadhalilishaji na wanyonyaji.
Kuna njia za kuwashirikisha watoto katika kujilinda na ukatili na udhalilishaji, lakini hii ni mada ya siku ingine, ila kwa leo Kumbuka, Kinga Kabla ya Tiba!
Leave a Reply