mtoto.news

Kajiado: Vituo 94 vya Watoto Wanaotoroka Ukeketaji na Ndoa za Mapema

June 21, 2022

Mashirika ya kijamii (CSOs) katika kaunti ya Kajiado yameanzisha vituo 94 vya uokoaji kwa watoto wanaoepuka mila mibaya kama vile Ukeketaji (FGM) na Ndoa za Mapema katika kaunti hiyo.

Katika kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika, Mkurugenzi wa Kitaifa wa Compassion International Kenya, Samuel Wambugu alisema kwamba, vituo hivyo ni muhimu katika kuelimisha jamii juu ya madhara ya mila hizo.

“Tunatambua pengo kubwa la taarifa kuhusu mila potofu dhidi ya watoto na jinsi zinavyoathiri watoto nchini kote. Mashirika ya Kijamii hushirikiana na serikali na Mashirika ya Kitaifa ya Watoto katika kuendesha elimu ya kiraia katika kaunti nzima,” akasema.

Hafla hiyo ilifanyika katika shule ya Msingi ya Elangata Wuas huko Kajiado mnamo Alhamisi tarehe 16 mwezi Juni.

Siku ya Mtoto wa Afrika (DAC) huadhimishwa kila mwaka, mwezi Juni, tarehe16.

Siku hii pia inaadhimisha watoto waliofariki walipokuwa wanaandamana kupinga mfumo wa ubaguzi wa rangi wakati wa maasi ya Soweto nchini Afrika Kusini mwaka 1976.

Kaulimbiu ya mwaka huu ni ‘Kuondoa mila potofu zinazoathiri watoto: Maendeleo ya sera na utendaji tangu mwaka wa 2013’.

Kajiado ni miongoni mwa kaunti za Kenya ambako mila kama vile ukeketaji na ndoa za utotoni bado zimekita mizizi katika jamii.

Vituo hivi vya uokoaji, vimesaidia katika kulinda na kusaidia watoto ambao wamekabiliwa na mila mbaya. Wambugu alielezea. 

Alisema kuwa, midahalo ya jamii imeanzishwa ambayo inahakikisha kuwa, Umma unafahamishwa kwamba, vitendo hivyo ni ukiukwaji wa haki za binadamu na za kimsingi.

“Vitendo viovu huathiri sana makuzi ya watoto na wakati mwingine hata kusababisha kupoteza maisha na lazima tuhakikishe kuwa, hakuna mtoto anayepitia lolote kati ya hayo,” alisema.

Sio wasichana pekeyake ndio walio hatarini kutokana na mila hii mibaya’ Esther Kuriat, Mkurugenzi wa Compassion International anasema.

“Wavulana katika kaunti ya Kajiado pia wanakabiliwa na changamoto ya kazi za mapema kama vile ujenzi kwani wanalazimika kutunza familia zao na kuacha shule,” alisema.

Wambugu aliongeza kunena kuwa, Mswada wa Watoto kwa sasa katika Seneti utasaidia sana ulinzi wa watoto nchini Kenya.

Pia aliwapongeza wadau wa jamii kama walimu na wazee wa jamii ambao kwa ujasiri walishawishi hasa kwa ajili ya sera na mazoea yanayohimiza kukomeshwa kwa vitendo hivi hatari katika jamii yao.

Mkurugenzi Msaidizi wa Baraza la Taifa la Huduma za Watoto Mary Thiong’o alisema kuwa Baraza hilo linaendelea na uhamasishaji wa watendaji na wadau wote ili kuhakikisha watoto wanalindwa dhidi ya ukeketaji na ndoa za utotoni.

Aidha, Bunge la 12 limepitisha muswada wa sheria ya watoto Leo hii, Tarehe 17 mwezi juni mwaka wa 2022 Nchini Kenya, ambao tutauita Sheria ya Mtoto Mwaka 2022.

Mwandishi-Khadija Mbesa

Hey, like this? Why not share it with a buddy?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *