mtoto.news

Waziri wa Elimu Atupilia Mbali Mada ya Kuongezwa kwa Muhula

August 25, 2022

Waziri wa Elimu George Magoha amefutilia mbali kuongezwa kwa kalenda ya shule baada ya shinikizo kutoka kwa wakuu wa shule wa sekta ya elimu.

Akizungumza baada ya kufungua madarasa ya mtaala unaozingatia umahiri huko Njiru, Magoha alisema kuwa wizara ina nia ya kuhakikisha kalenda ya shule inarudi kuwa ya kawaida mnamo Januari.

Alisema kuwa kufikia sasa, hakuna mipango ya kurekebisha kalenda hata katikati ya mazingira ya kisiasa yasiyo ya uhakika.

“Kila mtu anaonekana kuwa na wasiwasi wa kuongezwa kwa muhula, ila kwa tathmini yangu shule nyingi zimeshamaliza silabasi, na kwa sasa wanazingatia marudio,” alisema

Magoha alithibitisha kuwa mitihani ya kitaifa itasimamiwa jinsi ilivyoratibiwa.

Shule zinatarajiwa kugharamia muda uliopotea katika wiki nne zijazo, kwani muhula wa pili unatarajiwa kumalizika Septemba 16.

Waziri wa elimu pia alisema kuwa serikali iko mbioni kutekeleza madarasa ya shule za upili kwani kaunti nyingi zimekamilika kwa asilimia 85.

Aliwataka wasimamizi wa shule kutomrudisha mwanafunzi yeyote nyumbani kwa kukosa karo na badala yake washirikiane na mzazi.

Pia alinena kuwa shule katika maeneo manane ya uchaguzi ambapo uchaguzi unatarajiwa kufanyika Jumatatu zitasalia kufungwa kwa siku moja tu.

“Watoto wanaobaki shuleni, kuna mengi ya kufanya, unaweza kufanya mijadala au kucheza uwanjani na wanaoenda nyumbani, basi unaweza kusoma vitabu,”  Magoha aliwanasihi wanafunzi.

Hey, like this? Why not share it with a buddy?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *