mtoto.news

Tuwaepushe watoto kutokana na dhuluma na habari potovu mitandaoni.

September 2, 2022

Waziri wa mawasiliano Joe Mucheru amewalaumu wazazi kwa kukosa kukagua wavuti wanazoingia watoto wao. Alisema haya mwaka jana katika hafla ya uzinduzi wa programu ya kuwalinda watoto mitandaoni, iliyoasisiwa na Mama wa Taifa, Bi Margaret Kenyatta jijini Nairobi.

Aliongezea alisema kuwa, kuweka nywila(pini) kwenye simu na vifaa za wavuti, sio suluhisho tu ya kuwalinda watoto kutokana na dhuluma mitandaoni. “Hatuwezi kuwalaumu watoto wetu. Lawama ni kwa wazazi ambao mara nyingi huwa wazembe baada ya kuwapa watoto wao simu. Ni jukumu letu sote kupambana na dhuluma za watoto mitandaoni. Wazazi lazima wawe katika mstari wa mbele katika kutekeleza hilo,” akashauri Bw Mucheru.

Pia alihusisha mavazi mabaya, matumizi ya lugha chafu, mitindo inayokiuka tamaduni za kiafrika na vifo miongoni mwa watoto na ukosefu wa wazazi kuweka mipaka katika habari wanazofaa kuzitazama watoto wao.

Akiongezea, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mawasiliano, Mercy Wanja alisema matumizi ya mtandao yameongezeka kwa asilimia nne mwaka jana kutokana na janga la corona.

Aidha, amewataka wazazi kuhakikisha kuwa watoto wanapata tu fursa ya kufikia wavuti zinazohusiana na elimu bali si za kuwapotosha.

“Uzinduzi wa kampeni hii ni njia ya kuwalinda watoto wetu. Hatutaki wafikie habari za kuwapotosha,” akasema Bi Wanja.

Hata hivyo, Bi Wanja alisema watashirikiana na walimu na Taasisi ya Mtaala (KICD) ili kuunda wavuti itakayoangazia masuala ya watoto na kuwapa mafunzo ya kiakademia.

Alisema wanashirikiana na wadau mbalimbali kama vile Wizara ya Elimu, KICD, Ofisi ya wapelelezi wa makosa ya jinai na mahakama kuu ili kuwachukulia hatua watakaopatikana wakiwadhulumu watoto mtandaoni.

Jaji Mkuu, Martha Koome ambaye pia alihudhuria hafla hiyo alisema tayari wameunda programu mtandaoni itakayotumika kurekodi kesi zote na kuwawezesha polisi kufuatilia kesi zote za dhuluma.

Dhuluma na habari potovu mitandaoni imeweza kuwaadhiri watoto kwa njia mbalimbali. Baadhi ya watoto hawa wameweza kuwa na fikra za kujiua, kutojithamini, kuwa na upweke, wasiwasi na huzuni. Shida hizi zimeweza kuwaadhiri shuleni na pia katika maisha yao ya kila siku.

Kwa hivyo, serikali, wazazi na walezi wanafaa kuweka mikakati nzuri Ili kuwaepusha watoto kutokana na dhuluma na habari potovu mitandaoni. Watoto pia wanafaa kuwa makini na kuangalia vitu zinazowahusu na kuwasaidia katika mitandao.

 

Hey, like this? Why not share it with a buddy?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *