Vifo vya karibu watoto 100 nchini Indonesia vimesababisha nchi hiyo kusimamisha uuzaji wa dawa zote za sharubati.
Ni wiki chache tu baada ya dawa ya kikohozi nchini Gambia kuhusishwa na vifo vya karibia watoto 70.
Indonesia imesema kwamba, baadhi ya dawa za sharubati zimepatikana kuwa na viambato vinavyohusishwa na majeraha ya figo (AKI), ambayo yameua watoto wadogo 99 mwaka huu.
Haijabainika iwapo dawa hiyo iliagizwa kutoka nje au ilitengezwa nchini.
Siku ya Alhamisi tarehe 20 mwezi wa Kumi 2022, maafisa wa afya wa Indonesia wamesema walikuwa wameripoti takriban visa 200 vya AKI kwa watoto, wengi wao wakiwa na umri wa chini ya miaka mitano.
Mapema mwezi huu, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitoa tahadhari ya kimataifa kuhusu dawa nne za kikohozi ambazo zilihusishwa na vifo vya karibu watoto 70 nchini Gambia.
WHO iliweza kugundua kwamba, syrups zilizotumiwa Gambia zilizotengenezwa na kampuni ya dawa ya India, zilikuwa na “kiasi kisichokubalika” cha diethylene glycol na ethylene glycol. Dawa hizo “zina uwezekano wa kuhusishwa na majeraha ya figo”, lilisema shirika hilo.
Waziri wa Afya wa Indonesia siku ya Alhamisi alisema kwamba, misombo hiyo hiyo ya kemikali pia ilipatikana katika baadhi ya dawa zinazotumiwa nchini humo.
“Baadhi ya syrup ambazo zilitumiwa na wagonjwa wa watoto wa AKI chini ya miaka mitano zilithibitishwa kuwa na ethylene glycol na diethylene glycol ambazo hazikupaswa kuwepo, au za kiasi kidogo sana,” alisema Budi Gunadi Sadikin.
Hata hivyo, hakufichua ni kesi ngapi zilizohusisha dawa hizo zenye sumu.
Mamlaka ya Indonesia ilisema kwamba, dawa za kikohozi zinazotumiwa nchini Gambia hazikuuzwa nchini humo.
Mtaalamu mmoja alisema kuwa, idadi ya vifo inaweza kuwa kubwa zaidi kuliko ilivyoripotiwa.
Mamlaka ya Indonesia hadi sasa haijafichua chapa au aina za dawa za syrup zinazohusishwa na watoto wagonjwa, badala yake zimepiga marufuku kwa muda uuzaji na maagizo ya dawa zote za syrup na za maji maji (Kioevu).
Leave a Reply