Suala la changamoto za ulinzi wa watoto katika jamii na shule ni jambo la kusikitisha mno, kwani mara nyingi wanafunzi ndio waathiriwa, huku wahusika wakuu wakiwa walimu wao. Kati ya mwaka wa 2014 na 2019, takriban walimu 125 kwa mwaka waliachishwa kazi na Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) kwa sababu ya unyanyasaji wa kijinsia shuleni.
Mnamo mwaka wa 2009, TSC iliripoti kuwa, ndani ya kipindi cha miaka mitano wasichana waliofika 12,660 walinyanyaswa kingono na walimu wao, ila licha ya hayo ni walimu 633 pekee walioshtakiwa kwa unyanyasaji wa kijinsia katika kipindi hicho, na kesi nyingi hazikuripotiwa. Rekodi kutoka TSC hazikuwa wazi kuhusu idadi ya wasichana wa shule waliodhulumiwa lakini ripoti hiyo ilisema kuwa katika visa vingine,walimu waliwanyanyasa hadi wasichana 20 katika shule moja kabla ya kuripotiwa.
Mnamo 2019, TSC iliripoti kuwa, imewafuta kazi walimu 1,228 wa shule za msingi na upili katika miaka saba iliyopita kwa sababu ya kuwadhulumu kingono wanafunzi. TSC ilikiri kwamba kesi nyingi zaidi haziripotiwi kwa sababu baadhi ya tamaduni huchochea ndoa za utotoni, huku wazazi walio hatarini wakikubali pesa za kimyakimya kutoka kwa wakosaji.
Tafiti nyingi zimefanywa kuhusu unyanyasaji wa kijinsia wa wanafunzi na walimu nchini Kenya. Utafiti mmoja kama huo mnamo mwaka 2014 uliwahoji wanafunzi 500, ambapo asilimia 57.6 ya waliohojiwa walichukulia unyanyasaji wa kijinsia katika Kaunti ya Makueni kuwa ‘juu’ huku asilimia 10.2 pekee ndio waliona kuwa unyanyasaji wa kijinsia ni wa chini.
Utafiti huo pia ulionyesha kuwa ni asilimia 10 pekee ya visa vya unyanyasaji wa kijinsia vinavyoripotiwa kwa TSC, na hata kati ya hizo zilizoripotiwa, ni asilimia 70 tu ya walimu waliofukuzwa kazi au kustaafu, huku asilimia 30 wakihamishwa kwa taasisi zingine.
Mbali na masuala ya ulinzi wa watoto na kuhatarisha watoto kuripotiwa shuleni, tafiti zimeonyesha kuwa tishio hilo pia limeenea katika jamii. Utafiti uliofanywa mwaka wa 2019 na Wizara ya Kazi na Ulinzi wa Jamii unaopima kuenea, asili na matokeo ya unyanyasaji wa kimwili, kihisia, na kingono dhidi ya watoto na vijana, ulibainisha kuwa, baadhi ya mienendo hasi ambayo imeandikwa katika ‘Ripoti ya Uchunguzi wa Ukatili Dhidi ya Watoto. – 2019’.
Mara nyingi, wahusika wa unyanyasaji wa kijinsia huwa familia ya karibu na jamii, kwani utafiti huu wasema kwamba, miongoni mwa asilimia 15.6 ya wanawake waliofanyiwa ukatili wa kijinsia utotoni, karibu theluthi mbili (asilimia 62.6) walipata matukio mengi kabla ya umri wa miaka 18. Kwa wanawake, watu wa karibu ndio wahusika wa kawaida wa ukatili wa kijinsia wa utotoni, unaojumuisha asilimia 44.4 ya matukio ya kwanza. Wanawake wawili tu kati ya watano waliofanyiwa ukatili wa kijinsia utotoni ambayo ni sawa na asilimia 41.3, walimwambia mtu kuhusu tukio hilo la unyanyasaji wa kijinsia.
Isitoshe, janga la Covid-19 lilizidisha hali hiyo kwani kufungwa kwa shule na kuanzishwa kwa kufanya kazi nyumbani kuliwaweka watoto wengi hatarini, hasa wale wanaotangamana na wanyanyasaji wa ngono majumbani. Takwimu za Ofisi ya Kitaifa ya Takwimu ya Kenya zinaonyesha kuwa unyanyasaji uliongezeka kutoka 5,397 mwaka wa 2019 hadi 6,801 mwaka wa 2019, hii ikionyesha ongezeko la asilimia 26.
Mitindo na takwimu hizi zinapaswa kuwa chanzo cha wasiwasi kwetu. Nina furaha kutambua kwamba serikali imetayarisha Mpango wa Kitaifa wa Kuzuia na Kukabiliana na Ukatili dhidi ya Watoto wa 2019-2023. Mpango huu unajumuisha maeneo sita ya kimkakati: Sheria na Sera; Msaada wa familia , ambao ni ujuzi wa uzazi na uimarishaji wa kiuchumi;Elimu na stadi za maisha; Kanuni na maadili ya jumuiya; Majibu na huduma za usaidizi; na Uratibu.
Mpango huu unachukua mtazamo wa jamii nzima kwani kuzuia na kukabiliana na ukatili kunahitaji ushirikishwaji wa sekta zote, watoto wenyewe, vijana, wazazi, walezi, familia na jamii. Sekta za kibinafsi na zisizo za kiserikali pia hazijaachwa nyuma.
Kwa hakika nchini Kenya,tunaelekea katika njia ifaayo, lakini mengi zaidi yanahitajika kufanywa ili kuweka mazingira salama ambapo watoto wetu wanaweza kujifunza na kukua.
Leave a Reply