Mwinjilisti aliye na utata nchini Kenya, ameondolewa mashtaka ya ulanguzi wa watoto kutokana na ukosefu wa ushahidi wa kutosha.
Hakimu wa Kenya alieleza kwamba, upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha kuwa Gilbert Deya aliwaiba watoto watano miongo miwili iliyopita, . Mwinjilisti huyo alishutumiwa kwa kuwakabidhi watoto hao kwa wanawake waliokuwa wakihangaika kupata mimba.
Mchungaji huyo alihamishwa kutoka Uingereza mwaka wa 2017, baada ya vita vyake vya kisheria vilivyodumu kwa muongo mmoja kushindikana. Wasiwasi uliibuliwa kwa mara ya kwanza kuhusu mwenendo wa Bw Deya, ambaye alikuwa akiendesha kanisa moja mjini London, katika uchunguzi wa BBC mwaka wa 2004.
Wanawake waliokuwa na matatizo ya kupata mimba ambao walihudhuria kanisa la Gilbert Deya Ministries huko Peckham, kusini-mashariki mwa London, waliambiwa wangeweza kupata watoto wa “miujiza”. Lakini watoto hao mara zote “walinyakuliwa na kuibwa” katika kliniki za mtaani ndani ya mji mkuu wa Kenya, Nairobi. Upande wa mashtaka ulisema kwamba, watoto hao waliibwa kutoka kwa familia maskini za Kenya.
Katika uamuzi wake siku ya Jumatatu, hakimu Robison Ondieki alisema kwamba, upande wa mashtaka “umeshindwa kupata ushahidi wa kimazingira”.
Akizungumza nje ya mahakama ambapo wafuasi wake walimshangilia, Bw Deya alisema kuwa amewasamehe waliotaka kumuona jela. “Leo nimeachiliwa kwa mzigo wa aina hii, nira begani mwangu… iliyoharibu sifa yangu,” aliwaambia waandishi wa habari, na kuongeza kuwa “inasikitisha kwamba nimebandikwa kama mwizi wa watoto”.
“Ninashukuru kwamba niko huru. Sasa nitaendelea na utume ambao Yesu alinipa duniani.” Alidokeza kuwa anaweza kutaka kurejea Uingereza.
Mnamo 2011, Mary Deya, mke wa wakati huo wa Bw Deya, alifungwa jela baada ya kupatikana na hatia ya kuiba mtoto kutoka hospitali kuu ya rufaa katika mji mkuu wa Kenya Nairobi na kudai kuwa alikuwa amejifungua mtoto huyo.
Leave a Reply